Saturday, June 2, 2012

Serikali yakwama kuwavunjia waliojenga ufukweni



Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
Serikali imekwama kutekeleza zoezi la kubomoa nyumba zote zikiwemo hoteli zilizojengwa mita 60 kutoka fukwe za Bahari ya Hindi ndani ya wiki mbili kama ilivyokuwa imeahidi baada ya kubainika kwamba wamiliki wa maeneo hayo wana vibali halali kutoka Manispaa husika.

Mapema mwezi huu Mawaziri wawili walikutana na waandishi wa habari na kutoa tamko la pamoja ambapo waliwapa wiki mbili wamiliki wote waliojenga nyumba ndani ya mita 60 kutoka fukwe za bahari kuzibomoa.


Mawaziri waliotoa msimamo huo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Therezya Hivisa.


Katika tamko hilo viongozi hao walisema wameamua kutoa tamko hilo ili kulinda fukwe za Bahari kwa madai kuwa kujengwa kwa makazi na sehemu za biashara kunaharibu mazingira.


Hata hivyo, jana Dk. Huvisa alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya utekelezaji huo, alisema zoezi hilo limekuwa gumu baada ya kubainika kwamba wamiliki wa nyumba wana vibali halali walivyopewa na Manispaa husika na kuongeza kuwa suala la kubomoa hoteli linahusu wizara nyingine inayohusika na utalii.


Kwa upande wake, Profesa Tibaijuka alisema serikali imeanza kusoma ramani za fukwe ambapo imebaini kuna watu wamevamia maeneo hayo na kujenga makazi pamoja na sehemu za biashara.


Aliongeza kuwa wameshaanza kazi za upigaji picha katika fukwe hizo na kwamba baadhi ya watu wamemilikishwa maeneo hayo isivyo halali.


Profesa Tibaijuka katika agizo hilo ambalo lilitolewa kati kati ya mwezi uliopita alisema hatua hiyo ya bomoabomoa ilitolewa na serikali ili kulinda mazingira ya nchi nzima na fukwe kwa ujumla ambazo alisema hivi sasa zimevamiwa


Wakati huo huo, Dk. Hivisa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema siku ya mazingira kitaifa mwaka huu itaadhimishwa mkoani Kilimanjaro Juni 5, mwaka huu ambapo kauli mbiu ni uchumi kijani unakuhusu?

No comments:

Post a Comment