Saturday, June 2, 2012

Vigogo 11 wasimamishwa kazi Halmashauri ya Sengerema


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
Siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Erika Musika, kwa ubadhirifu, madiwani wa halmashauri hiyo wamewasimamisha kazi watumishi 11wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za miradi ya maendeleo.

Hata hivyo, madiwani hao wamewasamehe watumishi 13 baada ya kubaini kuwa hawahusiki licha ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwataja kuhusika katika ubadhirifu huo wa Sh. bilioni 2.4.

 
Uamuzi huo ulichukuliwa na madiwani hao baada ya kupitia barua zao za utetezi kwa mujibu wa maelekezo ya Pinda yaliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo, Mei 8, mwaka huu kuwa madiwani watapitia utetezi wa kila mtuhumiwa na baadaye kuwachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwaburuza mahakamani.
 
Maofisa waliosimamishwa kazi na madiwani hao kupitia kikao cha Kamati ya Maadili na idara zao katika mabano ni Paphili Masashua (Kilimo na Mifugo), Deusi Gelanizya (Mweka Hazina), Elikalia Edward (Mhandisi wa Maji), Mohamedi Kubelwa (Mhandisi wa Ujenzi), Onesmo Birago (Mipango),  Ofisa Maendeleo ya Jamii ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Zabuni, Lameck Butoto na Mabula Mnyeti (Ardhi).
 
Wengine ni ofisa ugavi wilaya aliyetajwa kwa jina moja la Lugakila, Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa M azingira Serengerema (Suwasa) Thomas Mwenda, Mwanasheria wa Halmashauri, Sifael Miguli huku mmoja wa wahandisi wa ujenzi, Wawa Nyonyori  na mhasibu wa Suwasa, Masebu Lupoja, wakiandaliwa mashitaka.
 
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mathew Lubongeja, alisema kwa mujibu wa maagizo ya mkuu wa mkoa, watuhumiwa hao watafikishwa kwenye kamati ya maadili cha mkoa na makati ya ushauri ya mkoa kujadiliwa.
 
“Sisi hatuna mamlaka ya kuwachukulia hatua isipokuwa tumewasimamisha kazi hadi maamuzi yatakapotolewa na kikao cha maadili cha mkoa ambapo watajadiliwa na baadaye watachukuliwa hatua,” alisema Lubongeja.
 

No comments:

Post a Comment