Saturday, June 2, 2012

JK ampa Mama Kanumba Sh. milioni 10

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete
Baada ya serikali kukabidhi rambirambi iliyoahidi ya Sh. milioni 10 kwa mama mzazi wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba, mama huyo anatarajia kuhama Sinza kwenye nyumba aliyokuwa akiishi mwanaye.

Mama Kanumba alikabidhiwa fedha hizo nyumbani kwake jana na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amosi Makala, zinatokana na ahadi iliyotolewa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, aliyoitoa wakati wa msiba wa Kanumba.

Wakati akipokea fedha hizo mbele ya mwanasheria wa wizara ya michezo, na kamati ya mazishi, mama Kanumba alisema anatarajia kuhamishia vitu vya mwanae Temeke anapoishi yeye kutoka mahala hapo alipoanza kuishi baada ya kifo cha Kanumba.

"Nitarudisha vitu vya mwanangu Temeke, wakati anahamia Sinza mwaka 2010, alikuwa anaishi Temeke chini ya uangalizi wangu, na hapa kodi ya pango imeisha," alisema mama huyo aitwaye Flora Mtegoa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati akikabidhi kiasi hicho cha fedha,
Makala alisema serikali imetekeleza ahadi iliyotolewa wakati wa kifo cha msanii huyo.

"Hii ni ahadi ya serikali iliyotolewa na rais wakati wa maandalizi ya mazishi ya Kanumba, tunaomba upokee kama pole ya msiba," alisema Makala.

Alisema serikali imejifunza mengi kupitia msiba wa Kanumba, kutokana na kwamba msanii huyo amefariki huku akiwa ametengeneza filamu 42, lakini alichopata hakilingani na kazi aliyofanya.

Kutokana na kuliona hilo, alisema wizara itafanyia kazi suala hilo la unyonywaji wa kazi za sanaa haraka iwezekanavyo ili wanufaike na jasho lao.

Naye Mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya msanii huyo, Mtitu Game, alishukuru serikali kwa kutoa msaada huo kwa Mama Kanumba, ambapo alisema wamefarijika kuona inawajali wasanii wake.

Aliishukuru pia wizara hiyo kwa kuahidi kufuatilia suala la uchakachuaji wa kazi za wasanii ambazo zinatengenezwa kila kukicha lakini wanaonufaika ni wengine.

Naye Mama Kanumba aliishukuru serikali kwa fedha alizopewa na kamati ya mazishi, ambayo ilifanikisha mazishi ya mwanaye.

"Sina cha kuwalipa isipokuwa nawaombea kwa Mungu," alisema Mama Kanumba.
Akizungumzia suala la urithi wa mali za mwanae, alisema bado hajafungua kesi ya usimamizi wa mirathi ya mali alizoacha mwanae.

"Bado sijafungua kesi ya msimamizi wa mirathi ya mwanangu ila baba Kanumba alituma watu waende mahakamani kufungua kuwa yeye ndiye msimamizi wa mali za Kanumba," alisema.

Hata hivyo, mama Kanumba alisema watu hao baada ya kwenda Mahakama ya Kinondoni waliambiwa waende Kisutu, lakini hadi sasa hajajua nini kinaendelea kwani hajapata taarifa yoyote kuhusiana na suala hilo.

No comments:

Post a Comment