Saturday, June 2, 2012

CHADEMA YASEMA HAIKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA CCM


Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakiko tayari wakati wowote, kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuunda serikali na kwamba hali hiyo ni usaliti kwa Watanzania.

Viongozi wakuu wa Chadema, Freeman Mbowe (Mwenyekiti) na Dk. Wilbrod Slaa (Katibu Mkuu)   wamesema hayo jana wakati wakizungumza na wananchi, walipofungua matawi ya chama hicho katika wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.

Mbowe na Dk. Slaa wanaongoza maandamano na mikutano ya hadhara yenye lengo la kuhamasisha vuguvugu la mabadiliko (M4C) kupitia Operesheni Okoa Kusini (Lindi na Mtwara).

Tandahimba ni miongoni mwa maeneo ya kusini mwa Tanzania ambako Chama cha Wananchi (CUF) kinachounda Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar, kina ngome zake.

Wakiwa katika tawi la Mihuta, Mbowe alisema serikali ya CCM imeshindwa kuyafikia matarajio ya umma, hivyo kuungana katika kuunda serikali, ni sawa na kuukubali unyanyasaji, ufisadi, matumizi mabaya ya rasilimali za umma na rushwa vilivyoshamiri kwa watawala.

“Chadema hatuwezi hata kwa wakati mmoja kuungana na CCM ili tuunde serikali, tunachotaka sisi ni kuiondoa CCM madarakani, hatuwezi kuingia kwenye ndoa ya kushika dola,” alisema.
Mbowe aliishambulia dhahiri CUF kwa hatua ya kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kwa kile alichosema inaashiria kushamirisha utawala wa CCM, licha ya kughubikwa na vitendo vya kifisadi.

Hata hivyo, Mbowe alisema kasoro iliyojitokeza ni kwa viongozi wakuu wa CUF katika ngazi ya kitaifa, lakini walio katika ngazi za chini kwenye jamii hawawezi ‘kubebeshwa msalaba’, bali kuunganisha nguvu na Chadema.

Naye Dk. Slaa alisema hali ya kisiasa na mwamko wa wananchi mkoani Mtwara, vimethibitisha kuwa Chadema inakubalika kwa umma, hivyo ni azma ya chama hicho kuendeleza vuguvugu la mabadiliko ili kuiondoa CCM madarakani na kuleta matumaini mapya kwa Watanzania.

“Tulipokuja mara ya kwanza mwaka 2004, tukapanda mbegu kwenye mikoa ya Kusini na baadaye wenzetu CUF wakawekeza huku, tuliamini kwamba mbegu ile ingezaa, haijakuwa hivyo,” alisema.

Alisema mbali na mikoa ya Kusini mwa nchi, Chadema iliwahi kupandikiza mbegu kwenye mikoa mbalimbali nchini ambapo mbegu ziliota na ‘kuzaa’ wabunge 49 na madiwani 560 waliopo sasa kupitia chama hicho.

Pamoja na maandamano na mikutano, Chadema inatekeleza mpango wake wa kufungua matawi kwenye kata tofauti, huku baadhi yakiwa ni yaliyokuwa ya CCM ama CUF.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment