Mawaziri wa ulinzi kutoka Sudan na Sudan Kusini wanaendelea na
kikao maalum mjini Addis Ababa, Ethiopia, kujadili masuala ya ulinzi na
usalama mipakani mwao kutokana na kuibuka kwa migogoro.
Mkutano huu, ukibarikiwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, AU, umeanza jana, huku wajumbe kutoka pande zote na viongozi wakuu wakikutana ili kuepusha kutokea kwa mapigano ya mpakani kwenye maeneo yanayogombaniwa, ambapo utata juu ya mipaka ya sasa na ile ya zamani likiwa tatizo kubwa.
Susan Rice, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wamezipa Sudan muda wa miezi
miwili, hadi Agosti 2, ziwe zimeshapata suluhu juu ya mambo kadhaa,
ikiwa ni pamoja na kuainisha mpaka wa kila moja, usafirishaji wa mafuta
na masuala ya uraia.Mazungumzo yanafanyika bila masharti
Mjumbe Amun ameongeza kuwa pande husika na jopo la mazungumzo wamekubali kutekeleza kikamilifu azimio namba 2046 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mpango wa Umoja wa Afrika.
"Tumekubaliana kuzungumza bila ya kuwa na masharti yoyote yale, pia Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika kwa pamoja wametuomba tufanye hivyo." Alisema Mjumbe huyo
Mjumbe huyo kutoka Sudan Kusini alisema kuwa jopo la usuluhishi la Umoja wa Afrika liliitisha mkutano tarehe 7 Juni kujadili juu ya jimbo la Abyei ambalo limekuwa chanzo kikuu cha uhasama baina ya Sudan na Sudan Kusini.
Anasema pande mbili zinajadili juu ya kuanzishwa utawala na mifumo mingine muhimu ya kurejesha amani jimboni humo.
Wananchi wa Sudan
Mazungumzo haya yalitanguliwa na shutuma wiki iliyopita, Sudan Kusini
ikiishtumu Sudan kwa kukataa kuondoa majeshi yake kutoka Abyei. Umoja
wa Mataifa ulikuwa umezipa nchi hizo hadi Mei 16 kuondoa majeshi yao
kutoka Abyei, lakini Sudan haikuondoa majeshi yake hadi tarehe Mosi
Juni.Sudan na Sudan Kusini zilipigana vita kwa muda mrefu na mwaka jana Sudan Kusini ikapata uhuru wake na kuwa taifa huru, lakini mwaka huu nchi hizo mbili ziliingia katika mapigano mara baada ya Sudan Kusini kuuteka Mji wenye utajiri wa mafuta wa Heglig, na baadae Sudan kuwafurusha askari walikuwepo katika mji huo na kusababisha vifo vya askari wengi katika mapigano hayo.
No comments:
Post a Comment