Monday, June 11, 2012

Taifa Stars lazima kieleweke kesho


Kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen
Sosthenes Nyoni
TIMU ya Taifa (Taifa Stars), kesho itahitaji umoja wenye uzalendo wa dhati toka kwa mashabiki wa soka nchini ili iweze kuifunga timu ya Taifa Gambia katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.Stars itangia dimbani ikiwa na majeraha ya kipigo cha mabao 2-0 walichopata toka Ivory Coast wiki moja iliyopita, hivyo ushindi kwenye mchezo wa kesho utaamsha faraja kubwa.
Baadhi ya mashabiki wa soka wamekuwa na utamaduni wa kuizomea timu hiyo katika baadhi ya mechi zake, na kwa kutambua hilo Kocha Kim Poulsen amewaangukia na kuwataka kuipa sapoti ili ishinde mchezo huo.
Wakati Stars ikisaka heshima kesho, mbabe wake Ivory Coast itakuwa dimbani leo kupepetana na Morocco iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 na Gambia katika mchezo wa kwanza.

Poulsen amesema atafanya mabadiliko kidogo katika kikosi chake kitakachoanza kwenye mchezo huo, akisema atampanga 'kiraka' Erasto Nyoni nafasi ya beki wa kati kuziba nafasi ya Aggrey Morris  anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu.
"Ni wazi nitalazimika kufanya mabadiliko kwenye safu ya ulinzi kwani tayari Aggrey Morris ana kadi nyekundi, bila shaka nafasi yake atacheza Erasto Nyoni. Ni mchezaji mzuri na mtulivu," alisema Poulsen.
Mabadiliko hayo yana maana kibarua cha kulinda lango la Stars kitakuwa mikononi mwa Nyoni na Kelvin Yondan watakaocheza kama mabeki wa kati, huku Amri Maftah na Shomari Kapombe wakicheza kulia na kushoto.
Eneo lingine ni safu ya ushambuliaji ambapo kiungo mshambuliaji Haruna Moshi'Boban' aliyekosa mechi dhidi ya Ivory Coast, anaweza kurudi   dimbani baada ya maendeleo ya afya yake kuzidi kuimarika.
Boban amerejea kwenye mazoezi baada ya awali kuondolewa kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja kama ilivyokuwa wenzake Nurdin Bakar na Said Nassoro'Cholo'.
Wakati huohuo, harakati hizo zitawashuhudia majirani wengine wa Tanzania, wakishuka dimbani leo ambapo Uganda (The Crance) iliyolazimisha sare ya bao 1-1 na Angola itakuwa mwenyeji wa Senegal kama ilivyo kwa Ethiopia itakayoumana na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Wanachama wengine wa Jumuhia ya Afrika Mashariki, Rwanda baada ya kuuumizwa mabao 4-0 na Algeria, kesho wataishukia Benin, wakati Sudan itakuwa ikivutana shati na Lesotho na Kenya ikiraruana na Namibia.


No comments:

Post a Comment