Baada
ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kumruhusu mtoto Saidi Adam (11)
kurejea nyumbani kutokana na tatizo linalomkabili kuonekana kuwa kubwa
kwao, hivi sasa mtoto huyo anahitajika kupatiwa matibabu nje ya nchi ili
kuokoa maisha yake.
Akizungumza na Nipashe Jumamosi jana, baba
wa mtoto huyo, Adam Said alisema kwa sasa wapo nyumbani kwa mwenyeji
wao Makonde Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, wakiwa hawajui la kufanya
kutokana na Muhimbili kushindwa kutatua tatizo.
“Tumeambiwa mirija ya kupumua na ile ya
maji kuelekea kwenye moyo imeziba, hivyo kusababisha tatizo la kukua kwa
moyo ambao sasa unaonekana umekuwa na mapacha,” alisema Adam.
Hata hivyo, Adam alisema baada ya kulazwa
kwa takribani siku 10 katika hospitali hiyo, madaktari walitoa dawa ili
ziweze kupunguza uvimbe wa tumbo, lakini si kwa kutibu tatizo
linalomkabili Said.
Alisema kutokana na tatizo hilo, anawaomba
wasamaria wema wajitokeze kumsaidia mtoto wake kuweza kusafirishwa nje
ya nchi kwa ajili ya kutibiwa tatizo hilo na aweze kurejea katika hali
ya kawaida.
“Kwanza kabisa nawashukuru watu mbalimbali
waliojitokeza kumsaidia Said kupitia kwa wahusika wa gazeti hili, na
wale ambao walinichangia ili kuweza kulazwa hospitalini kuangaliwa
tatizo lake..Mungu atawalipa zaidi na ninawaomba wengine wajitokeze
kufanya hivyo,” alisema.
Alisema watu ambao wanahitaji kumsaidia
Saidi ili kumwezesha kufanikisha matibabu yake hususani nchini India,
wanaweza kutumia akaunti namba 0152303111100 CRDB tawi la Mikocheni kwa
jina la Hadija Abdallah Mkwinda, ama ofisi za gazeti hili.
Saidi ni mtoto kutoka kijiji cha Mbaya
wilayani Liwale mkoani Lindi ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa moyo
tangu Agosti 2008 na kumsababishia tumbo lake kukua siku hadi siku.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment