MKUU
wa Mkoa wa Tanga, Chiku Gallawa, amepiga marufuku magari ya mizigo
kubeba watu kwenda kwenye mikusanyiko ya watu wengi, ikiwamo misibani na
harusini lengo likiwa ni kuepusha maafa yanayotokana na ajali.
Agizo
hilo limekuja baada ya kukithiri kwa vifo vitokanavyo na ajali za
barabarani, ambazo husababishwa na magari ya mizigo kubeba watu kwenda
misibani, maharusini na minadani. Mwaka jana watu 24 walipoteza maisha na wengine 39 kujeruhuiwa na kupata ulemavu wa maisha. Akizungumza
kwenye kikao cha wadau wa usafirishaji na wamiliki wa magari ya mizigo
juzi, Gallawa alisema kuanzia sasa ni marufuku magari ya mizigo kubeba
watu na kuwapeleka katika mikusanyiko.
Gallawa alisema imekuwa
kawaida kwa watu wa Tanga kutumia magari ya mizigo kwenda katika
shughuli za jamii na kusahau maafa ambayo yanaweza kutokea, huku
wakiacha usafiri wa mabasi.
“Kuanzia sasa ni marufuku kwa magari
ya mizigo kubeba watu na kuwapeleka katika sherehe au misibani,
tunashuhudia maafa ya mara kwa mara yanayotokana na ubebaji watu kwenye
malori, sasa basi!” alisisitiza Gallawa.
Aliwata wakazi wa mijini
na vijijini kuacha kutumia usafiri huo, kwani umekuwa ukipoteza roho za
watu wengi na watumie mabasi ambayo ndiyo wenye haki za kisheria kubeba
abiria. Kuhusu tabia ya baadhi ya madereva kuweka miti na majani
barabarani gari linapoharibika, Gallawa alisema watu hao wamekuwa
wakichafua mazingira kwani gari hilo likitengenezwa hawaondoshi uchafu
huo.
Alisema tabia hiyo imekuwa kero na wakati mwingine
husababisha ajali bila sababu za msingi, hivyo kila kijiji kinatakiwa
kuwa na walinzi ambao watanakili namba za magari yanayofanya hivyo. |
| |
No comments:
Post a Comment