Mzee Bob Makani
MWASISI
wa Chadema na Mwanasheria mkongwe nchini Bob Makani, amefariki dunia
usiku katika hospitali ya Aga khan, jijini Dar es Salaam.
Habari
zilizopatikana na kuthibitishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto
Kabwe, Makani alizidiwa ghafla saa 3: 00 usiku wa kuamkia leo na
kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alifariki dunia saa 4.15
usiku.
“Amekuwa anaumwa muda mrefu, mara kadhaa akipelekwa
hospitali na baada ya muda anaruhusiwa, lakini hii ya sasa alikua
nyumbani akazidiwa ghafla wakampeleka hospitali na ilipofika saa 4.15
wakasema amefariki,” alisema Zitto.
Zitto alisema kuwa, suala la
wapi utakapozikwa Makani ambaye ni Katibu Mkuu wa Kwanza na Mwenyekiti
wa pili wa Chadema, litajulikana baada ya kujadiliana na familia ya
marehemu.
“Suala la wapi atazikwa kama ni Shinyanga ama Dar es
Salaam, litajulikana baada ya kuzungumza na familia yake, kwa sasa
tunashughulika kwanza na kuhifadhi mwili wa mzee wetu,” alisema Zitto. Zitto alisema msiba wa utakuwa nyumbani kwa marehemu eneo la Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Kwa
siku za hizi karibuni afya yake imekuwa ikizorota na kumfanya
kuripotiwa kuanguka mara kwa mara alipokuwa akifanya shughuli zake.
Januari
17 mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema
Regia Mtema, Makani alianguka muda mfupi baada ya kuuaga mwili wa
marehemu.
Baada ya tukio hilo, alibebwa na kupelekwa pembeni
ambako alipepewa kwa takriban dakika tano kisha kurejea katika hali yake
ya kawaida na kurudi kwenye kiti chake
Alikuwa Katibu Makuu wa
kwanza wa Chadema kati ya mwaka 1993 hadi 1998, alikuwa Mwenyekiti wa
chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa Jimbo la
Shinyanga Mjini kwa mara tatu kati ya mwaka 1995 na 2000 na mwaka 2005.
Kazi
ambazo amewahi kuzifanya serikalini; alikuwa naibu mwanasheria mkuu wa
serikali, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mwaka 1966 na
elimu yake ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu Cha Makarere nchini
Uganda.
Ni mzaliwa wa Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga akitokea kwenye ukoo wa kichifu wa Makani.
|
No comments:
Post a Comment