Ni
kazi ngumu kwa Taifa Stars kuibuka kiongozi wa Kundi C la michuano ya
awali ya Kombe la Dunia kanda ya Afrika kuliko ngamia kupita katika
tundu la sindano.
Lakini matumaini yoyote madogo yaliyopo
yatafutika kabisa kama timu ya taifa ya soka haitashinda mechi yake
nyepesi zaidi ya nyumbani ya kampeni hiyo.
Stars iliyofungwa mabao 2-0 na Ivory Coast
katika mchezo wa kwanza wiki-endi iliyopita ugenini, ipo kundi moja pia
na Morocco na Gambia inayocheza nayo leo kwenye Uwanja wa Taifa.
Na miongoni mwa timu tatu hizo, nchi hiyo
ya Afrika Magharibi ndiyo pekee inayoonekana kuzidiwa uwezo na Stars na
isingeweza kucheza nayo wakati muafaka zaidi ya sasa.
Ili kufufua matuamini ya kuongoza Kundi C
na kupata nafasi ya kuingia hatua ijayo ya mtoano ya michuano hiyo ya
awali, timu ya taifa ni lazima ishinde leo ili isijikute angalau pointi
nne nyuma ya timu iliyo kileleni, baada ya raundi mbili na baada ya
mchezo kati ya vigogo vilivyopo kundini.
Na ikiwa katika mazingira hayo inakutana
na Gambia ambayo ina rekodi nzuri kuliko Tanzania katika ngazi ya
michuano ya vijana ya FIFA ikiwa imecheza fainali tatu za dunia kati ya
2005-2009, lakini si kikosi cha kwanza.
Wasiwasi pekee unabaki kwenye malamiko ya
kocha Kim Poulsen aliyesema juzi kuwa amesikitishwa na kitendo cha
shirikisho la soka (TFF) kutompatia DVD za mechi za Gambia ili ziweze
kumsaidia katika maandalizi ya mchezo wa leo.
Pengine TFF ilikwaza na uchache wa mechi za kimataifa ambazo Gambia imecheza.
“Pamoja na kuzikosa DVD hizo nimekiandaa
kikosi changu kukabiliana na Gambia na naamini watatumia vizuri uwanja
wa nyumbani kwa kushinda mabao mengi,”alisema Poulsen kurejesha
matumaini kuwa Taifa Stars itafanya kweli katika mchezo wake pekee ambao
itaingia uwanjani ikipewa nafasi kubwa ya kushinda.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment