Viongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA)
Naibu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezrone Kaaya, alitangaza azama hiyo jana mjini Dodoma mbele ya wanahabari na kusema wanachosubiri ni kusikia kauli ya serikali kwenye bajeti ya Wizara ya Fedha iwapo imezingatia mapendekezo yao hayo.
Alisema wafanyakazi waliiomba serikali kuwapunguzia kodi ya pato la mshahara (Paye), kupandisha kima cha chini cha mshahara hadi kufikia 200,000 kwa mwezi kwa sekta ya umma na kurekebisha pensheni.
Katika masuala hayo serikali imezingatia moja la kuweka uwiano wa pensheni baada ya kuunda mamlaka ya kusimamia mifuko ya pensheni (Ssra).
“Tucta na vyama shiriki tulitaka makato ya Paye yashuke kutoka asilimia 15 hadi asilimia 9 , tulitoa mapendekezo ya namna ya kufidia pengo hilo miaka miwili iliyopita. Kodi hiyo imeshuka kwa asilimia moja tu tena mwaka jana,” alisema Kaaya.
Alisistiza zaidi kuwa, “ Tucta tunaweka wazi kuwa kama serikali haitazingatia maoni yetu yaliyotokana na majadiliano tusilaumiwe kwa hatua tutakazozichukua kwa kutumia silaha yetu ya umoja. Serikali itambue kuwa Tucta hatupendi kuharibu ….”.
Aliongeza kuwa wafanyakazi wataikaba koo serikali kwenye nyongeza ya mishahara na kodi ya mapato ya –Paye na kusisitiza “ Tucta tunahitaji mambo haya mawili yafanyiwe marekebisho katika bajeti ya mwaka 2012/13 vinginevyo utaibuka mgogoro mkubwa ambao serikali haitaweza kuuzima kirahisi.”
Alisema iwapo serikali haitazingatia maoni yao wanaanza vikao na maamuzi ya kuitisha mgomo nchi nzima yatafuata na safari hii hawatarudi nyuma kama ilivyotokea mwaka 2010.
Alisema Tucta itajiunga na walimu pamoja na madaktari kuendesha mgomo huo wa kitaifa na serikali isije kuwalaumu iwapo itapuuza mapendekezo ya wafanyakazi.
Waliulaumu hatua ya kuondoa kodi kwa makampuni kadhaa pia kwenye boda boda zinazomilikiwa na vigogo lakini kuwabandikia mzigo mkubwa wa kodi wafanyakazi hatua ambayo alisema haitakubalika wala kuvumilika tena.
No comments:
Post a Comment