Tuesday, July 17, 2012

Changamoto kwa wakimbizi Sudan Kusini


Mkimbizi Sudan Kusini

Shirika la kushughulikia maslahi ya watoto, Save the Children, limeonya dhidi ya kukithiri kwa idadi na matatizo ya wakimbizi katika eneo la mpakani kati ya Sudan na Sudan Kusini.,

Kwa mujibu wa shirika hilo, makabiliano katika mpaka huo unaozozaniwa na nchi hizo mbili, yamesababisha ongezeko la wakimbizi wakiwemo watoto 2,000 wanaowasili katika kambi zilizojaa watu Kusini mwa Sudan karibu kila siku.

Vurugu nazo zimechacha kwenye mpaka huo tangu Sudan Kusini kujipatia uhuru mwaka jana.

Mashirika ya kutoa misaada yameonya kuwa hali huenda ikawa mbaya sana katika kambi hizo za wakimbizi.
Mapema mwezi huu, maafisa wa shirika la misaada ya kimatibabu la MSF, walisema kuwa wakimbizi wameanza kuambukizwa magonjwa hatari kwa sababu ya hali wanamoishi katika kambi za wakimbizi.

Inaarifiwa kuwa idadi ya vifo katika kambi ya Jamam , mojawapo ya kambi tatu zilizoko katika jimbo la Upper Nile, nusura kufikia zaidi ya idadi inayohitajika ili kutangaza janga la kibindamau.


Maelfu ya familia zinaendelea kuwasili katika kambi kila siku , wakiwa na njaa pamoja na hofu ya kutembea kwa siku nyingi ili kufika maeneo salama, hii ni kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la Save the Children Sudan Kusini.

"Watu wanakuja huku mvua kubwa inayonyesha ikifanya hali kuwa ngumu kwa mashirika ya misaada kuweza kufika maeneo yanayohitaji msaada. Tunashuhudia hali mbaya sana ya kibinadamu katika mojawapo ya maeneo duni sana duniani" alisema mkurugenzi huyo.

Tangu Sudan Kusini ilipojitenga na Sudan mwaka jana mapigano yamezuka katika miji miwili ya mpakani kati ya nchi hizo mbili, ambako jamii ambazo zinaishi maeneo ya Kusini zilijipata Kaskazini mwa mpaka baada ya uhuru.

No comments:

Post a Comment