Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka imeendelea kuimarika baada ya kupata matibabu nchini Afrika Kusini na sasa figo zake zimeanza kufanya kazi.Dk Ulimboka alipelekwa
nchini huko mwishoni mwa wiki baada ya kushambuliwa na watu
wasiojulikana kiasi cha kusababisha figo zake kushindwa kufanya
kazi.Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangila alisema Dar es Salaam jana kwamba, hali ya Dk Ulimboka imeimarika na kuwaomba Watanzania wamuombee apone haraka.“Taarifa tulizozipata kutoka Afrika Kusini zinasema kwamba, hali ya Dk Ulimboka imezidi
kuimarika tofauti na alivyokwenda, figo zimeanza kufanya kazi ingawa
kwa polepole na amefanyiwa vipimo vingine,” alisema Dk Kabangila na kuongeza:“Pia ameanza kuzungumza, anawatambua watu vizuri na zaidi amewaomba Watanzania wamuombee apone haraka.” Awali, chanzo kimoja cha habari kilidokeza kwamba hali ya Dk Ulimboka imeimarika
kutokana na kupatiwa huduma za matibabu kwa haraka kwa kufanyiwa pamoja
na vipimo vingine, kile cha usafishaji damu na figo (Dalysis), mara kwa
mara. Kabla ya kuondoka nchini, Dk Ulimboka alifanyiwa usafishaji huo mara mbili.
Madaktari
walisema kuwa, kipimo hicho kililenga kupunguza kiwango cha sumu
iliyoonekana kwenye damu, ambayo haikutambulika mara moja kama
ilitengenezwa ndani ya mwili au vinginevyo kwa kuwa hakuna kipimo cha
kubaini tatizo hilo nchini.
Migomo hospitalini Licha ya huduma
kurejea taratibu katika baadhi ya hospitali nchini, mgomo wa madaktari
bingwa umeendelea chini kwa chini.Pia jana, Serikali imewataka madaktari
wote walio katika mafunzo ya vitendo kuripoti Wizara ya Afya na Ustawi
wa Jamii, ifikapo Ijumaa.
Jana, wizara hiyo ilitoa taarifa
ikitaka madaktari wote nchini wanaofanya mafunzo kwa vitendo (interns)
ambao walipewa barua za kurudishwa wizarani, kuripoti Dar es Salaam Julai 6, mwaka huu.
Mgomo
wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH),
umekuwa na utata baada ya kuwapo taarifa mbili zinazokinzana.
Uongozi
wa (MNH) kupitia kwa Msemaji wake, Aminiel Aliegaeshi umetoa taarifa
kwa umma kupitia vyombo vya habari jana ukisema huduma za matibabu
zinaendelea kama kawaida, lakini kwa kiwango cha kati.
“Huduma
hapa hospitalini zinaendelea kutolewa kwa kiwango cha kati, wagonjwa ni
wachache wanaokuja kutibiwa. Madaktari Bingwa wote wameingia na
kufanya kazi na Interns kumi na moja wamefanya kazi,” alisema.
Jana
waandishi wetu walishuhudia baadhi ya huduma zikiendelea kutolewa kama
kawaida katika hospitali hiyo zikiwemo x-ray katika Taasisi ya Mifupa
(Moi) na hospitali hiyo kuu.
Awali, huduma hiyo na nyingine zilisimama baada ya tukio la kutekwa na kupigwa kwa Dk Ulimboka.
Lakini,
wakati Aliegesha akitoa taarifa hiyo, madaktari bingwa wamesisitiza
kuwa wako kwenye mgomo huku msemaji wao, Dk Cathrine Mng’ong’o akitaka
waandishi wa habari kulinganisha maneno hayo ya uongozi na hali halisi
hospitalini hapo.
“Mimi siwezi kujibu swali hilo (kama wako kwenye mgomo au wamerudi), sababu sipo katika eneo la hospitali
leo, niko nyumbani. Wewe angalia kwa macho yako uone kisha linganisha
maneno hayo na hali halisi,” alisema Dk Mng’ong’o.Alipoulizwa kuwa kama
jana alikuwa zamu alijibu kwa kifupi kuwa madaktari bingwa hawana zamu
na hufanya kazi saa 24.
Madaktari hao juzi walitangaza mgomo wakitaka Serikali kuwarudisha kazini madaktari wote waliofukuzwa.
Uongozi
wa MNH ulisema, idara ambazo madaktari walikuwapo ni ya huduma za
dharura na katika vitengo vingine ilidaiwa kuwa walifika kwa kiwango
kikubwa.
Katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru,
hali imezidi kuwa tete baada ya wagonjwa kuhamishiwa hospitali za
binafsi kutokana na kuzorota kwa huduma.Mkazi wa Sakina
aliyejitambulisha kwa jina moja la Manka, ambaye mtoto wake alikuwa amelazwa hospitalini hapo akisubiri upasuaji alisema, amelazimika kumhamisha mtoto wake kutokana na kukosa huduma.
Hata hivyo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Eliringia Mlay alikanusha madai ya kuwapo kwa mgomo hospitalini hapo na kusema kuwa, ulikuwapo awali lakini kwa sasa umekwisha na madaktari wanaendelea na kazi kama kawaida. Hospitali binafsi
Hospitali
ya TMJ imeanza kutoa huduma ya tiba kwa baadhi ya wagonjwa waliokuwa
Muhimbili baada ya kuingia mkataba na Serikali ili kutoa huduma ya
matibabu katika kipindi ambacho madaktari wa Serikali wapo katika mgomo.
Msemaji
wa Hospitali hiyo, Huzaifa Seif alisema jana kuwa wagonjwa wanaotibiwa
katika hospitali hiyo ni wale wenye kadi za Bima ya Afya na wagonjwa
walioandikiwa rufaa kutoka MNH. Hata hivyo, mmoja wa wagonjwa, Anaeli
Mbasha alisema ingawa Serikali imeingia mkataba na hospitali hiyo,
wagonjwa wengine wenye kipato kidogo wanashindwa kuhimili malipo.
Hospitali ya Regency imekuwa na ongezeko la wagonjwa
ikiaminika kuwa ni kutokana na mgomo huo wa madaktari. Mmoja wa
madaktari hospitalini hapo, Dk Emmanuel Jonathan alisema wagonjwa ni
wengi hasa kutoka Muhimbili.
Katika Hospitali ya Aga Khan, baada ya wiki iliyopita kuwa na ongezeko la wagonjwa
kwa asilimia 15, idadi hiyo imepungua kati ya jana na juzi.Mkurugenzi
wa Tiba wa Aga Khan, Dk Jaffer Dharsee alisema: “Ongezeko kubwa lilikuwa
katika vipimo ambavyo vinapatikana katika Hospitali ya Muhimbili na
hapa (Aga Khan), peke yake kwa mfano MRI (Magnetic Resonance Imaging).”
Geofrey Nyang'oro, Victoria Mhagama, Halima Shebuge, Zakhia Abdallah, Sam Jacob (SJMC), Pamela Chilongola na Sam Jacob, Moses Mashalla, Arusha.
HABARI KWA HISANI YA GAZETI LA MWANANCHI |
No comments:
Post a Comment