Wednesday, July 4, 2012

Madaktari bingwa wagoma rasmi


Daktari Bingwa Catherine Mng’ong’o akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya msimamo wa madaktari bingwa kuwa hawako tayari kufanyakazi bila ya kuwepo wenzao waliofukuzwa.
Wakati serikali ikiendelea kuwatimua kazi madaktari katika hospitali za serikali nchini walioshiriki kwenye mgomo wa kutofanya kazi, madaktari bingwa nao wametangaza rasmi kuingia katika mgomo wa nchi nzima wakipinga hatua yake ya  kuwafukuza kazi wenzao.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais Jakaya Kikwete, kuwatangazia madaktari wote kusitisha mgomo na kurudi kazini mara moja kwa kuwa madai yao ya kuongezewa mshahara hayawezi kutimizwa na serikali.

Mwakilishi wa madaktari bingwa nchini, Dk. Catherine Mng’ong’o, wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema madaktari bingwa hawawezi kuendelea kufanya kazi bila kuwepo kwa madaktari wa chini.



Dk. Mng’ong’o, alisema madaktari bingwa wapo tayari kufukuzwa kazi kwa kugoma kama walivyofukuzwa madaktari wengine wanaofanya kazi katika hospitali za serikali nchini.

“Hatupo tayari kufanya kazi bila ya madaktari wanaofanya kazi chini yetu, kwa hiyo na sisi tupo tayari kuacha kazi,” alisema Dk. Mng’ong’o baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari hao uliofanyika Muhimbili kuanzia kuanzia asubuhi hadi mchana .

MUHIMBILI WAJISAJILI

Mapema jana asubuhi, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Dk. Marina Njelekela, alitoa tangazo lililobandikwa kwenye mbao za matangazo akiwataka madaktari wanaotaka kuendelea na kazi kujiandikisha kwa wakuu wao wa idara.

Kwa mujibu wa Dk. Njelekela zoezi hilo lilianza jana na limepangwa kufungwa leo asubuhi saa 3:00 na kwamba linawahusu madaktari wote wanaokuja kazini, lakini hawafanyi kazi.

“Wakuu wote wa Idara wanatakiwa kuwaorodhesha madaktari wote watakaofika kazini kuanzia leo (2/Julai/2012) na kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, na taratibu zilizopo…tangazo hili haliwahusu Madaktari walio katika Mafunzo kwa Vitendo (Interns),” alisema Dk. Njelekela na nakala ilipelekwa kwa wakurugenzi kwa usimamizi.

JUMUIYA YA MADAKTARI NA HOTUBA YA JK

Jumuiya ya Madaktari Nchini imesema hotuba iliyotolewa mwishoni mwa mwezi uliopita na Rais Kikwete haikuzungumzia namna serikali itakavyoboresha huduma za afya nchini.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk. Edwin Chitage, alisema msimamo wa madaktari kugoma utaendelea kama kawaida na kwamba wapo tayari kwa mazungumzo na Rais ili kujadili mambo ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na serikali.

“Sisi tupo tayari kufanya mazungumzo na Rais ili tujadiliane kuhusu madai yetu ambayo tunafikiri hayajaeleweka vizuri na tunataka tufanye hivyo kwa sababu tunaamini majadiliano ndiyo njia pekee ya kupata ufumbuzi,” alisema Dk. Chitage.

Dk. Chitage alionyesha kushangazwa na mtazamo wa baadhi ya wananchi kuwa madai ya madaktari yanalenga nyongeza ya mshahara siyo ya kweli na kwamba wanachodai ni uboreshwaji wa mazingira ya huduma za afya.

Alisema hospitali zote za serikali nchini hazina kipimo cha CT-Scan ambacho gharama yake siyo kubwa ikilinganishwa na matumizi mengine ya serikali.
Kuhusu kufukuzwa madaktari, Dk. Chitage alieleza  kushangazwa na uamuzi uliochukuliwa na serikali kudai kuwa suala la madaktari lipo mahakamani huku ikiendelea kuwafukuza ni uvunjaji wa sheria.

Alisema taarifa zilizopo ni kwamba hadi sasa zaidi ya madaktari 300 wa mazoezi wameshafukuzwa kwa kurejeshwa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakati suala hilo lipo mahakamani.

Dk. Chitage alisema kutokana na uamuzi ulioanza kuchukuliwa na serikali, baadhi ya madaktari wameanza kuandika barua za kuacha kazi wenyewe.

MOI, MUHIMBILI

Hali ya utoaji wa huduma katika Taasisi ya Mifupa (MOI), na ya Muhimbili imeendelea kuzorota na kuleta usumbufu kwa wagonjwa.

Mwanahamisi Jumbe mmoja wa wagonjwa waliofika MO , alisema alipewa ahadi ya kufika jana kupata huduma ya matibabu kutokana na ajali ya mguu, lakini hadi saa 5:00 hakuwa ameonana na daktari kwa kuwa bado mgomo unaendelea.

Hali ya huduma kwa ujumla kwenye hospitali hizo siyo ya kuridhisha kwa kuwa madaktari bado hawajarejea kazini.

M/NYAMALA YATIMUA 27

Madaktari 27 wa mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Mwananyamala wameondolewa na kurejeshwa mikononi mwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii baada ya kubainika kuwa wameshiriki mgomo.

Madakatari hao waliotimuliwa ni kati ya 51 wa vitendo waliopelekwa katika hospitali hiyo.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu wa Hospitali hiyo, Dk. Edwin Bisakala, alisema hatua hiyo imechukuliwa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kwamba daktari anayeendelea na mgomo aache kazi au aondolewe.

Dk. Bisakala, alisema madaktari 24 waliobakia, uongozi wa hospitali hiyo utaendelea kufuatilia utendaji wao wa kazi kama una ufanisi na ikibainika umezorota hatua zitachukuliwa kwa kuwarejesha wizarani kama wenzao.

Alisema pamoja na mgomo wa madaktari unaoendelea hakuna mgonjwa aliyepewa rufaa ya kwenda hospitali binafsi na kwamba huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.

Alisema hospitali ina wagonjwa 344 waliolazwa ambao wanaendelea na matibabu.

AMANA SHWARI

Katika hospitali ya Amana, huduma zimeendelea kutolewa kama kawaida huku baadhi ya madaktari wakiripotiwa kutofika kazini.

Daktari kiongozi wa hospitali hiyo kitengo cha dharura, Dk. Christopher Mnzava, alisema idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepungua kutoka wagonjwa 10-15 kwa siku hadi wagojwa 3-4 kwa siku tangu mgomo ulipoanza.

Dk. Mnzava alisema utekelezaji wa agizo la Rias Kikwete utafanyika baada ya kufanya tathmini ya mahudhurio ya saa 24 kwa siku ya jana.

DODOMA, MOSHI

Madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, wameendelea na mgomo wao kama kawaida huku wakipinga kitendo cha serikali kuwapa vitisho.

Hospitali hiyo ambayo ina jumla ya madaktari 250 kwa idara zote, lakini kutokana na mgomo huo hadi sasa madaktari wanaotoa huduma ni 15 kutoka nje ya nchi pamoja na watawa, hatua ambayo imesababisha huduma kwa wagonjwa wa nje kufungwa.

Wakizungumza na NIPASHE walisema lengo lao la kuendelea na mgomo siyo kuwakomoa wananchi ili wapoteze maisha bali ni kuishinikiza serikali kuboresha huduma za afya nchini kwa kuongeza vifaa tiba na dawa.

“Takwimu za kiwango cha mshahara kilichotajwa na Rais Kikwete ni kutuchonganisha na wananchi, ili waone tunadai fedha nyingi wakati ukweli unafichwa, mshahara ni majadiliano kama sisi tumesema hivyo serikali imesema kiwango kipi?” alihoji mmoja wa madaktari.

Alisema suala la kuandika barua za kuacha kazi ni jambo ambalo haliwezekani kwani serikali ndiyo imewaandikia barua za kuwaondoa kwenye vituo vya kazi na kama wameona hawafanyi kazi basi wawafukuze, lakini msimamo utaendelea kuwa ule ule na wanafanya hivyo kwa kuwa wana uzalendo na nchi yao.

Alisema kitendo alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, kimewatisha na kuwadhalilisha madaktari wote nchini na siku zote kwenye viapo vyao vya kazi daktari anapaswa kumuona daktari mwenzake kama ndugu hivyo hawawezi kurejea au kufanya kazi ilhali mwenzao anateseka.

Kutokana na mgomo kuendelea huduma kwa wagonjwa wa nje imesitishwa katika hospitali hiyo isipokuwa kwa wale wanaokuja kuchukuwa dawa za sukari na kurefusha maisha (ARV).

Mkoani Dodoma, madaktari tisa kati ya 11 waliokuwa wamepewa barua za kufukuzwa kazi wamerejeshwa huku wawili wakirudishwa wizarani.

Hata hivyo, taarifa zinaeleza kwamba hakuna mgomo na madaktari wanaendelea na kazi kama kawaida.

MBEYA- RC AOMBA MSAADA JWTZ


Utoaji wa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya zimeendelea kusuasua kutokana na uhaba wa madaktari.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abas Kandoro ambaye jana alitembelea hospitali hiyo, alisema anakusudia kuomba madaktari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ili wasaidie kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi hospitalini hapo.

“Kwa kuwa Rais jana (juzi) aliwataka madaktari warudi kazini na leo (jana) madaktari hao hawaonekani nadhani sasa inabidi niwaombe wadaktari wa JWTZ kutoka kwenye vikosi vilivyo mkoani hapa waje hospitali na kusaidia kutoa huduma,” alisema Kandoro.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Eliuter Samky, alisema madaktari waliokuwa kwenye mgomo waliondolewa na kurudishwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.

“Hakuna hata daktari mmoja aliyekuwa kwenye mgomo ambaye leo ameripoti kazini, lakini kwa kuwa wale wote waliokuwa kwenye mgomo tuliwaondoa kazini kwa mujibu wa sheria za kazi na kuwataka warudi kwa Katibu Mkuu wa Wizara, inawezekana waliondoka kwenda Dar es Salaam,” alisema Dk. Samky.

Dk. Samky alisema kuwa hali ya utoaji wa matibabu Hospitalini hapo siyo ya kuridhisha na alisema kuwa Idara zilizoathirika zaidi ni ya upasuaji ambayo imebakiwa na madaktari wachache ambao hawawezi kufanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa.

Alisema kuwa Idara ya macho imebakiwa na daktari mmoja na Hospitali ya Rufaa ya Wazazi iliyopo eneo la Meta mjini hapa nayo imebakiwa na daktari bingwa mmoja, ambaye hawezi kabisa kukidhi mahitaji ya wagonjwa.

Dk. Samky alitoa wito kwa kina mama ambao wanasumbuliwa na magonjwa ya kawaida yasiyohitaji huduma za daktari bingwa kwenda kwenye hospitali nyingine kupata huduma badala ya wote kuelekea kwenye Hospitali ya Rufaa ya Meta.

Wakati huo huo, taarifa ya Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, kwa vyombo vya habari jana jioni ilieleza kwamba huduma katika hospitali hiyo zimerejea katika hali ya kawaida kwa maelezo kwamba madaktari wamerejea kazini jana.

Ilieleza kuwa tathimini iliyofanyika kuanzia saa mbili hadi saa 11 jioni inaonyesha kuwa katika idara zote madaktari walifika kazini isipokuwa waliokuwa likizo.
Iliogeza kuwa idara ya tiba yenye madaktari bingwa 21, 19 kati yao walifika kazini ambapo watatu wako likizo.

Aidha Registrars wote 12 walikuja kazini na kliniki zote za tiba zimefanyika kama kawaida.

“Katika Idara ya watoto, yenye madakatari bingwa 16, kati yao 14 walikuja kazini wengine wawili wako likizo na registrar watatu kati ya sita walikuja kazini ambapo watatu wako likizo…upande wa OPD yenye registrars saba, sita kati yao walikuja kazini na mmoja yuko likizo.

Aidha madaktari bingwa wote walikuja kazini,” alisema Aligaesha.

Alisema idara ya magonjwa ya afya ya akili yenye madakatri bingwa 10, tisa walifika  kazini na mmoja ambaye hakufika yuko masomoni.

Alisema kwa upande wa huduma za dharura, registrars wote 10 walifika kazini.

Kuhusu huduma za upasuaji, alisema wagonjwa wote waliolazwa wodini walionwa, na baadhi ya kliniki za huduma ya upasuaji zilifanyika.

Hata hivyo, upasuaji haukufanyika kwani hakukuwa na orodha ya wagonjwa waliopangwa kufanyiwa upasuaji. “Kwa ujumla madaktari wamerejea kazini,”

Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Ninaeli Masaki, Leonce Zimbandu, Yoramu Mrobezi, Dar; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Salome Kitomari, Moshi na Paul Mabeja, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment