Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk. Stephen Ulimboka.
Shtuma hizo zimetolewa jana na Msemaji wa kambi ya upinzani wa ofisi ya Rais, Profesa Kulikoyela Kahigi, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12 na Makadirio ya Mapitio na Matumizi ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2012/13.
“Hivi usalama wa taifa na vikosi vyote vya ulinzi na usalama vilikuwa wapi hadi wahabeshi wakavuka mpaka na kuendelea na safari hadi Kongwa,?” alihoji Profesa Kahigi na kuongeza:
“Kitendo cha kutekwa na kuteswa kwa kiongozi wa Chama cha Madaktari Nchini Dk. Stephen Ulimboka, na vyombo vya usalama vipo dhahiri kuwa hali ya usalama ni ya mashaka.”
Alisema hali ya usalama ni tete pia katika mipaka ya mikoa ya Kigoma na Kagera hususani kuhusiana na wahamiaji haramu.
Alisema kambi hiyo inayasema hayo kwa kuwa Rais ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa vyombo vyote vya usalama hapa nchini lakini kwa matukio hayo, Ofisi ya Rais haijatoa kauli ya kina bungeni ni kwa vipi watu hao wameingia toka nje na wanasafiri hadi katikati ya nchi bila kujulikana.
“Au kuna mtandao wa vyombo vya usalama unaojihusisha na biashara hiyo ya kusafirisha watu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi yetu?” alihoji.
Alisema huo ni udhaifu mkubwa kwa idara ya usalama wa Taifa na kuhoji ni kutokana na watendaji kupata kazi bila ya kuzingatia vigezo na weledi au kutojua umuhimu wa maana halisi ya idara hiyo kwa taifa.
Alisema tatizo la rushwa linaloigusa serikali ndio msingi wa pendekezo la kambi ya upinzani kuhusu kufanya maboresho ya Idara ya Usalama wa Taifa.
Alisema taarifa kubwa kama kashfa ya rada, rushwa ya Richmond, sakata la EPA na Ufisadi wa IPTL ni ishara kuwa idara ya usalama ni ya baadhi ya viongozi wa serikali, chama na familia zao.
Aidha, alisema kambi ya upinzani inaitaka serikali kutoa taarifa kwa Bunge kuhusu uchunguzi wa ubadhirifu wa kashfa ya Kagoda, Meremeta na Deep Green.
TAKUKURU
Profesa Kahigi alisema kambi hiyo inapendekeza kuwa uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ufanywe na Kamati ya Taifa ya Uteuzi na ithibitishwe na Bunge.
Kambi hiyo ilitaka taarifa za taasisi hiyo ziwasilishwe bungeni kila mwaka na kujadiliwa na Bunge kama ilivyosasa ambapo taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Halikadhalika, kambi hiyo imehoji ni hatua gani ambazo Takukuru wameshachukua juu ya tuhuma dhidi ya Jairo na wenzake ambazo zilithibitishwa na Kamati ya Bunge.
CHANZO:
NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni
No comments:
Post a Comment