Saturday, July 28, 2012

Uandikishaji Vitambulisho vya Taifa Dar kizungumkuti


 
MCHAKATO wa uandikishaji wa Vitambulisho vya Taifa jijini Dar es Salaam umeingia dosari, baada ya baadhi ya waandikishaji na maofisa wa serikali za mitaa kuwatoza wananchi fedha kinyume cha sheria.Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi  katika maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam umebaini kuwa, mfumo wa utambuzi umekuwa ukitumiwa na baadhi ya maofisa na viongozi wa serikali za mitaa kuwatoza wananchi fedha.

Hali hiyo imewakatisha tamaa baadhi ya watu na kuwafanya wahoji kama kuna kitu watakosa wasipokuwa na kitambulisho hicho.Mpango huo mbaya ya kuwatoza fedha wananchi  unafanywa wakati ambapo Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) inasisitiza kuwa uandikishaji huo ni bure na kuwa mwananchi yeyote hapaswi kutozwa fedha au gharama nyingine zozote.

Wananchi kadhaa waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana na juzi, jijini Dar es Salaam, walithibitisha kwamba walitozwa kati ya Sh500 na 3,000. Baadhi ya wakazi wa maeneo ya Temeke, Ilala na Kinondoni walilalamika kuwa, maofisa waandikishaji wanawatoza kati ya Sh500 na 1,000 ili waandikishwe.

Uchunguzi huo umebaini pia kuwa, maofisa wa ofisi za kata na mitaa wanatoza fedha kati ya Sh1,000 na 3,000 kwa watu ambao hawana vitambulisho, kama vile kadi ya mpigakura, cheti cha kuzaliwa, ubatizo au hati ya kusafiria.

Baadhi ya maofisa waandikishaji wanadaiwa kuwa, wanawaelekeza baadhi ya watu kwenda kupata barua ya za utambulisho katika ofisi za serikali za mtaa, au mtendaji ili kuthibitisha kuwa wao ni raia.

Baadhi ya wananchi wanadai walilipa fedha walizodaiwa kwa vile zoezi hilo ni mpango uliowekwa na Serikali.

Hata hivyo, imebainika kuwa wale ambao hawana uwezo waliacha kujiandikisha kwa imani kuwa hakuna watakalopoteza au kupata wakiwa na vitambulisho hivyo vya taifa, au wasipokuwa navyo.

Ashura Ally (32) mkazi wa Tabata Kisiwani wilayani Ilala, ambaye ni mmoja wa waliotakiwa kutoa fedha na ofisi ya serikali za mtaa alisema: “Mimi sina kitambulisho wala kitu chochote, lakini tatizo ni kuambiwa nikienda serikali za mitaa kuandikiwa niwe na Sh3000. Siwezi kutoa.”

Mkazi mwingine wa Tabata, Neema Shao (28) alilalamika kutumia muda mwingi kwenye foleni akisubiri kujaza fomu ya uandikishwaji. “Mtu mmoja anatumia dakika zaidi ya kumi kuandikishwa. Baadhi ya watu wameondoka kwa sababu ya kusubiri muda mrefu,” alisema Neema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Wailes, Abdon Kidege  alisema changamoto kubwa anayoiona ni watu kupuuzia zoezi la uandikishaji. “Baadaye tuliamua kuanza kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kazi hii. Walidhani ni jambo la kawaida tu lakini baada ya hapo walianza kujitokeza,” alisema.

Wakati huohuo, Mzee Rajabu Hakungwa (72) mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa iliyopo Tandika  alisema kuwa, wakazi wa eneo hilo hawakuwa na elimu juu ya umuhimu wa kuandikisha.

“Awali, wakazi wa mtaa wetu hawakutambua umuhimu wa zoezi hili,  lakini baada ya kuelimishwa kwa sasa wanaongezeka,” alisema Mzee Hakungwa.

Mkazi wa Tabata Kimanga, Prasido Kombe alisema huenda muda uliowekwa na Nida usitoshe kutokana na uandikishaji kwenda polepole.

“Tunaiomba Nida iongeze muda kwani tunasikia siku ya mwisho kujiandikisha ni Jumapili.  Kama itakuwa hivyo na kasi ya watendaji ni ndogo watu wengi watakosa nafasi ya kujiandikisha,” alilalamika Kombe.Mkazi mwingine wa Tabata Kisiwani, Abduly Juma alisema bado wananchi hawana elimu ya suala hiyo ndiyo maana wengi wao wamekuwa wakipuuzia kwenda kujiandikisha.

Kauli ya NIDA
Msemaji wa Nida, Rose Mdami alisema kuwa mwananchi yeyote hapaswi kutoa fedha yoyote ili kufanikisha mkakati wa kuandikishwa, hivyo akawaonya maofisa waandikishaji na wale wa  serikali za mitaa kuacha tabia hiyo.

Alisema Nida imekuwa ikifuatilia kwa karibu utendaji huo na kukiri kuwa dosari hizo zipo na baadhi maofisa wamewatia mbaroni.

“Tumefanikiwa kumkata mmoja wao katika Kituo cha Yombo Buza kilichopo Mtaa wa Sigara, Kata ya Tandika wilayani Temeke,” alisema Mdami. Imeandikwa na Aidan Mhando, Kelvin Matandiko na Zakhia Abdallah. 
  chanzo gazeti la mwananchi

No comments:

Post a Comment