Mkutano ukiendelea Bungeni
DK SLAA AONYA HAKUNA HURUMA, MSEKWA ASEMA RUSHWA ADUI WA HAKI, MBATIA ATOA WIKI MOJA SPIKA AWATAJE WOTE Kizitto Noya, Dodoma na Leon Bahati, Dar VYAMA
vya CCM na Chadema vimetoa onyo kali kwa wabunge wanaotuhumiwa kwa
kashfa ya kuhongwa na baadhi ya kampuni za mafuta na kulihujumu Shirika
la Umeme Tanzania (Tanesco), vikisema havitasita kuwawajibisha pindi
tuhuma hizo zitakapothibitika.Kauli ya vyama hivyo imekuja siku
moja baada ya wabunge watano, watatu wa CCM na wawili wa upinzani
kudaiwa kuhusika na vitendo hivyo vya rushwa, ambavyo vimesababisha
Spika wa Bunge, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili majina ya wahusika
yawekwe hadharani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa juu wa vyama hivyo walisema wanasubiri kwa hamu taarifa rasmi kutoka bungeni.
CCM: Rushwa adui wa haki Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa alisema chama hicho kimewaapiza wanachama wake wote kutotoa wala kupokea rushwa.
Alisema rushwa ni kosa la jinai hivyo anaamini vyombo husika vya dola vitachukua hatua zinazofaa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Katibu
wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikazia kauli hiyo akisema
rushwa inaelezwa katika katiba ya chama hicho kwamba ni, ‘adui wa haki’
na wanachama wote waliapishwa kuwa hawatapokea wala kutoa rushwa. Alisema yeyote anayekwenda kinyume na kanuni za CCM, anajiweka katika kundi la wasaliti wa chama.
Alisema
wabunge ni kundi maalumu nchini ambalo linalipwa vizuri ili lisimamie
vyema misingi ya maendeleo ya nchi pasipo tamaa wala vishawishi hivyo
wanapotajwa miongoni mwa kundi la wala rushwa, CCM kinalaani vikali
tukio hilo.
Kuhusu tuhuma hizo kutajwa kuwahusisha wabunge watatu
wa chama hicho, Nape aligoma akisema habari hizo siyo rasmi, hivyo
hawezi kuzizungumzia.
Hata hivyo, alisema CCM kinasubiri uchunguzi
ufanyike ambao ndiyo utakaoweka bayana wahusika wa tuhuma... “Tusubiri
uchunguzi ukamilike. Idadi inawezekana ikawa hiyo au ikapungua au
kuongezeka.”
Dk Slaa: Hatufumbii macho ufisadi Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema: “Nalaani kitendo cha
wabunge kuhusishwa na ufisadi hasa ikizingatiwa kwamba Chadema tumekuwa
tukiupinga vikali. Tumekuwa tukipinga rushwa kwa sababu ndiyo
inayoielekeza nchi pabaya… Chadema hatufumbii macho rushwa.”
Alisema
tangu kuanza Bunge la 10, Chadema kimekuwa kikiona baadhi ya mambo
yanayoendelea katika mhimili huo muhimu wa dola yamejaa walakini...
“Ndiyo maana sisi Chadema tumekuwa tukisema Bunge limepoteza mwelekeo.”
Alisema
akiwa mtendaji mkuu wa chama, anasubiri taarifa kamili kutoka katika
kikao cha wabunge wa chama hicho ili kuweka wazi majina ya wahusika na
kisha kufuatiwa na kikao cha Kamati Kuu (CC) ambacho kitakaa na kuchukua
hatua kali.
“Tunahitaji tupate maelezo ya kina... chama chetu
hakikurupuki… Nasubiri taarifa ya kokasi ya chama. Katiba ya Chadema
inatambua uwapo wa kikao cha wabunge wetu na kwa bahati nzuri, kiongozi
wake mkuu ni Mwenyekiti wa Chadema (Freeman Mbowe) na katibu (David)
Silinde ni mbunge wetu. Tunasubiri taarifa yao.”
Alisema Chadema
kina kanuni ya kudhibiti rushwa hivyo, mbunge wake akitajwa miongoni mwa
wanaohusishwa na rushwa, atawajibishwa kupitia kikao cha CC ya chama
hicho. NCCR-Mageuzi yakoleza moto
Katika hatua nyingine,
Chama cha NCCR- Mageuzi jana kilikoleza moto baada ya kumtaka Spika Anne
Makinda awataje wabunge hao bungeni ili wafukuzwe na kufungwa kama
Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inavyotaka.
Chama hicho
kimetoa wiki moja kwa Spika Makinda kufanya hivyo, kikionya kuwa
vinginevyo, chenyewe kitawasilisha hoja mahususi kutaka Bunge lichukue
hatua hiyo.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alitoa tamko
hilo mjini Dodoma, akisema Sheria Namba 3 ya Haki, Kinga na Madaraka ya
Bunge ya mwaka 1988, inataka wabunge wanaothibitika kujihusisha na
rushwa wafukuzwe na kufungiwa kwa kipindi cha miaka mitano.
“Ni
aibu kwa Bunge, taasisi inayoitwa tukufu kuwa na mafisadi. Kitendo cha
Spika kukubali kuivunja Kamati ya Nishati na Madini na kuahidi kuzivunja
nyingine, maana yake anakubali kuna mafisadi. Sisi tunamtaka atutajie
wabunge hao bungeni ndani ya juma moja,” alisema Mbatia.
Mbatia
aliyeongozana kwenye mkutano huo na wabunge Moses Machali wa Kasulu
Mjini na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini), alisema pamoja na Bunge
kuendeshwa kwa kanuni zake, kwa Tanzania kuwa mwanachama wa Jumuiya ya
Madola inaweza pia kuiga yaliyofanywa katika nchi nyingine za jumuiya
hiyo, zikiwamo India na Uingereza.
Kwa mujibu wa Sheria
zinazotumika katika nchi hizo, mbunge yeyote anayethibitika kutumwa na
mtu nje ya Bunge, kuongea au kuandika bungeni kwa masilahi ya mtu huyo,
anapaswa kufukuzwa ubunge na kufungwa.
“Kati ya mwaka 1924 na
1956, Uingereza ilifukuza wabunge 59 na kati ya mwaka 2005 hadi sasa,
Bunge la India liliwafukuza wabunge 11 baada ya kuthibitika walihongwa
na wafanyabiashara kuuliza maswali binafsi,” alisema.
Mbatia
aliendelea kueleza kuwa katika Bunge la Nane nchini, wabunge wanne
walikamatwa na kushtakiwa, kisha chama chao CUF, kiliwazuia kujihusisha
tena na siasa baada ya kubainika kuwa walifunga ndoa batili na Wasomali
ili wapate hati ya kuishi nchini.
“Sasa suala hili, wabunge wote
wanaohisi wamo kwenye orodha hii ya ufisadi waachie ngazi. Mbunge yeyote
na wa chama chochote anayeona ameshiriki uchafu huu, kwa utashi wake
aachie ngazi,” alisema na kuongeza: “Kwa vile vyama viadilifu, waige
mfano wa CUF. Bunge lichukue nafasi yake kabla hatujafunga Bunge Agosti
18 tuwe tumefanya uamuzi wa kuwafukuza.”
Mbatia alisema ili Bunge
lilirudi kwenye heshima yake, Spika Makinda pia anapaswa kuzitaja kamati
nyingine alizosema zinachunguzwa na ikiwezekana nazo zivunjwe ili haki
itendeke.
“Sisi (NCCR-Mageuzi) tunataka pia Spika azitaje kamati
hizo, ziko sita na tuseme pia kwamba hatuna imani na Kamati ya Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge. Tunataka nayo ijisafishe kwanza kwa kuwa
nako kuna watuhumiwa.” “Katika hili niombe kiti cha Spika kitende
haki, hata kama kuna mbunge wa NCCR-Mageuzi anahisi alishiriki ufisadi
huu, awahi mapema kuondoka, hii isiwe kwa vyama vingine tu,” alisema.
Mbatia
alisema suala la Tanesco ni tone tu, akisema ufisadi kwa wabunge
ulianza siku nyingi na kuongeza... “Mheshimiwa Kafulila (David)
aliwataja wajumbe wa Kamati ya LAAC lakini, mpaka leo hakuna
kinachoendelea.”
Alisema tatizo la ufisadi kuhusisha wabunge
lilianza Juni 23, 2006 siku ambayo nchi iliingia mkataba na Kampuni ya
Richmond... “Kuanzia hapo kumeendelea kuwa na sintofahamu katika Wizara
ya Nishati na Madini. Dawa yake ni kuweka mikakati ya Bunge kujitakasa.”
Sakata lenyewe Wabunge
hao watano (majina tunayahifadhi kwa sasa) wanatuhumiwa kutumia nafasi
zao za uwakilishi bungeni au ujumbe ndani ya kamati husika, kufanya
biashara na Tanesco na kutetea mafisadi wanaolihujumu shirika hilo
kutoka ndani na nje.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge waliochangia
hoja hiyo bungeni walisema wanawafahamu wabunge hao kwa majina, lakini
wasingependa kuwataja kwa kuwa siyo wakati mwafaka.
Moto wa kutaka kutajwa kwa majina ya wabunge hao ulikolezwa na Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita Kawawa ambaye aliomba Spika avunje Kamati ya Nishati na kutaka pia Bunge lijadili kashfa hiyo.
“Waheshimiwa
wabunge wamejadili suala hili kwenye wizara, lakini kwa mujibu wa
Kifungu cha 55 (3) f, Mbunge au Waziri anaweza kutoa hoja ili jambo
fulani lijadiliwe.
Sasa mimi naomba kutoa hoja ya kujadili suala
hilo.”Baada ya hoja hiyo kuungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge , ndipo
Spika Makinda aliposimama na kukubali hoja hiyo ya Mbunge Vita Kawawa
na kutangaza kuivunja kamati hiyo.
Spika Makinda alisema tayari
pia, ameagiza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutengeneza
kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia hiyo ya kupokea rushwa kutoka
kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi. “Nasema kwa
dhati kabisa kitendo hiki hakikubaliki ndani ya Bunge. Wabunge mkae
vizuri, kama kuna baadhi yetu wanakwenda huku na huku kujitafutia
masilahi binafsi mnawezaje kuisimamia Serikali?”
Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Seleman Zedi alisema
ameshtushwa na uamuzi huo wa Spika na kwamba anasubiri uamuzi wa Kamati
ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Akihitimisha hoja ya wizara
yake bungeni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
alisema baadhi ya wabunge ambao wanashiriki kwenye vikao vya uamuzi vya
Tanesco kama wajumbe wamekuwa wakilihujumu shirika hilo kwa njia
mbalimbali ikiwamo kufanya nalo biashara.
“Shirika liliwahi kulipa
Paundi 50,000 za Uingereza kwa ajili ya ununuzi wa vipuri, lakini
kilicholetwa nchini ni masanduku ya misumari. Nguzo hizo za umeme kuna
biashara inaendelea. Tunajua kwamba nguzo hizo zinazalishwa Iringa na
kupelekwa Mombasa kisha kurudishwa nchini kwa maelezo kwamba zimetoka
Afrika Kusini,” alisema Profesa Muhongo. |
No comments:
Post a Comment