Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30
Julai, 2012 kwa muda usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika
habari na makala za uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya
kusababisha wananchi kukosa imani na vyombo vya dola hali inayoweza
kuhatarisha amani na mshikamano uliopo nchini.
Katika matoleo yake hivi
karibuni, gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 –
18, 2012 na toleo Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na.
304 la Jumatano Julai 25 hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia
yamekuwa yakichapisha habari na makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa
jamii.
Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi,
ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya
makala zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya
taaluma ya uandishi wa habari.
Mhariri, mara zote katika utetezi
wake amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho
kinatoa uhuru wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30
cha Katiba hiyo kinachoweka ukomo wa uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali imeamua kulifungia
kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa
Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo
itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali
(Government Notice) Na. 258 lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na
kutolewa jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai, 2012.
Serikali inawataka wamiliki,
wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya
taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha,
kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.
Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati
wa kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
hivi karibuni waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha
kuwa habari wanazoziandika na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma
na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu na uzalendo. Uhuru na haki ya
vyombo vya habari uendane na wajibu.
Kuanzia sasa Serikali haitasita
kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa
taarifa za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu
uliopo nchini mwetu.
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment