Kizitto Noya, Dodoma SAKATA
la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari
Nchini, Dk Steven Ulimboka, limeibuka upya bungeni baada ya Kambi Rasmi
ya Upinzani, kuitaka Serikali itoe majibu ya kina kuhusu watendaji wake
kutajwa kuhusikana na tukio hilo.
Kambi hiyo pia imeitaka
Serikali ieleze sababu za watendaji hao kutokamatwa hadu sasa na
kuhojiwa na vyombo vya dola, wakati kuna taarifa kuwa wanafahamika.
Akiwasilisha
maoni ya kambi hiyo kuhusu hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, katia mwaka wa fedha wa 2012/13,
Conchesta Rwamlaza alisema, haiwezekani Serikali kuendelea kukaa kimya
wakati watendaji wake wanatajwa kuhusika katika tukio hilo.
Rwamlaza
alikuwa akizungumza kwa niaba ya msemaji wa kambi hiyo, Dk Antony
Mbassa, ambaye alitaka uchunguzi huru ufanyike kuhusu kubaini ukweli.
"Aidha
kwa kuwa Serikali imetuhumiwa kuhusika, kambi rasmi ya upinzani,
inasisitiza haja ya kuundwa kwa tume huru ili kufanya uchunguzi kuhusu
tukio hilo. Taarifa iliyotolewa na polisi kuhusu kukamatwa na kufikishwa
mahakamani kwa raia wa Kenya, haipaswi kutumika kama kisingizio cha
kuzuia mjadala na haiwezi kuwa kizuizi cha uchunguzi huru kuendelea
kufanyika," alisema Rwamlaza.
Katika hatua nyingine, Rwamlaza
alilaani kitendo cha Bunge kuzuia mjadala wa kibunge kuhusu tukio la
kutekwa kwa D Ulimboka, akisema hata kama limefanya hivyo kwa kutumia
kanuni, siyo sahihi. Kambi hiyo ilisema tukio la Ulimboka linapaswa
kufikishwa bungeni ili lijadiliwe na kwamba Bunge halipaswi kuwekewa
vikwazo vya kikanuni katika kujadili matatizo ya wananchi.
Kambi
hiyo ilienda mbali zaidi na kukituhumu kiti cha Spika kwamba kinachangia
mgogoro wa madaktari unaoendelea nchini, kwa kuzuia mijadala iliyoombwa
na wabunge kuhusu suala hilo ambalo hatima yake ni kuwasitishie leseni
madaktari 319.
"Kama Kiti kingetoa fursa kwa Bunge kujadili na
mwisho kutoa ushauri au maazimio yake kwa Serikali, jambo ambalo ndio
wajibu wetu kwa mujibu wa katiba ibara ya 63, mgogoro huo usingeendelea
kudumu kwa muda mrefu na kuleta athari zaidi katika sekta ya afya,"
alisema.
Rwamlaza alisema "kanuni zinazolizuia Bunge kujadili
masuala ya wananchi kwa kisingizio kuwa masuala hayo yako mahakamani,
zinadumaza demokrasia ya nchi yetu, zinalipora Bunge haki yake ya
kikatiba ya kuisimamia Serikali na zinawakandamiza wananchi wanyonge
ambao hawana pa kusemea isipokuwa kupitia Bunge lao."
Alielezea
kushangawa kwake na Bunge kuzuiwa kujadili suala hilo kwa maelezo kuwa
liko mahakamani, wakati Rais Jakaya Kikwete alilizungumzia katika hotuba
yake kwa taifa, ya Julai mosi mwaka huu. na kulitolea maagizo
mbalimbali.
"Kambi ya upinzani inataka kujua kama kitendo cha
Baraza la Madaktari Tanganyika kusitisha usajili kwa madaktari 319
kuanzia Julai 11 mwaka huu ni sahihi wakati madaktari hao walikuwa
wameshtakiwa mahakamani kwa shauri hilo," alisema.
Alisema
kutokana na upungufu huo, kambi ya upinzani inapendekeza Bunge liazimie
kuwa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma kwa Jamii,
iliyoshughulikia mgogoro kati ya Serikali na Madaktari, iwasilishwe
bungeni taarifa ya jambo hilo na kujadiliwa kabla ya kupitishwa kwa
bajeti ya wizara hiyo.
"Hatua hiyo italiwezesha pia Bunge
kupitisha maazimio ya kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu namna ya
kushughulikia vyanzo vya migogoro katika sekta ya afya," alisema na
kuongeza;
'Kitendo cha kuwadharau, kuwadanganya madaktari na
hatimaye kuwafutia leseni madaktari 319 wa mafunzo kwa vitendo, ni
kujikanganya kwa Serikal. Ni uamuzi unaoonekanaa umechukuliwa kwa
kukomoa na kwa ubabe bila kujali maslahi ya taifa na afya za wananchi. Mgogoro
mzima unaashiria uwezo finyu wa Serikali katika kutatua migogoro kwa
njia ya majadiliano na ukosefu wa dhima ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi
ya CCM," alisema.
Alisema kambi ya upinzania, inasikitishwa na
kitendo cha Serikali kushindwa kutumia busara katika kutafuta ufumbuzi
wa madai ya vitendea kazi na stahili za madaktari, jambo ambalo
lilisababisha migomo ya madaktari nchini.
Hata hivyo akiwasilisha
hotuba yake ya wizara bungeni jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii,
Dk Hussein Mwinyi, alisema Serikali imesikitishwa na tukio la kutekwa,
kuteswa na kutelekezwa msituni kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk
Steven Ulimboka.
"Serikali inatoa pole kwa ndugu Ulimboka na inamtakia kupona haraka ili aunganike na familia yake," alisema Dk Mwinyi.
Mapema
waziri huyo alieleza historia ya mgogoro wa madaktari na Serikali
akifafanua kuwa kwa upande wake, Serikali ilijitahidi kadri ilivyoweza
kuhakikisha kuwa unamalizika. Mwisho |
No comments:
Post a Comment