Tuesday, July 31, 2012

‘Tumieni vizuri siku zilizoongezwa’


 
Mwandishi Wetu
WAKAZI wa Dar es Salaam wametakiwa kuzitumia vizuri siku tano zilizoongezwa kujiandikisha katika suala la kupata vitambulisho vya taifa ili kuepuka matatizo yanaweza kujitokeza baadaye.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) ilipoelezea umuhimu wa wakazi wote halali kujiandikisha ili kupata vitambuilisho hivyo.

Ofisa Habari Mwandamizi wa Nida, Thomas William alisema Serikali imeongeza siku ili wote wenye haki ya kujiandikisha wafanye hivyo na kwamba  baada ya kumalizika siku hizo tano haitaongeza tena.

William aliwataka wakazi wa Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla kuwa wasikivu wanapoelezwa mambo ya kufanya kwa wakati husika.

“Suala la kujiandikisha lilianza siku nyingi, na wachache walikuwa wakijitokeza, lakini baada ya siku kumalizika makundi ya watu wanamiminika. Hii haifai, lazima tutumie muda kwa umakini”, alisema.

Alisema Nida inatarajia kufanya kazi hiyo kwa wakati na kwamba mpango huo ukifungwa Dar es Salaam Nida itaelekeza nguvu mikoa mingine na lengo ni kuhakikisha mchakato huo utakamilika kabla ya 2015.

Akifafanua kuhusu Dar es Salaam alisema Nida iliamua kuongeza siku kutokana na mwitikio wa wananchi siku za mwishoni .

"Mwishoni mwa wiki mwitikio ulikuwa mkubwa, hivyo itakuwa vizuri sana watu wakazitumia siku hizi za ziada kwa kasi kama walivyoonyesha ili kukamilisha mchakato na kila mmoja kupata haki yake ya kujiandikisha" alisema.
 William alisema changamoto  zinajitokeza wanajitahidi kuzitatua na kuzifanyia kazi na kwamba Jumatano ijayo watakuwa katika nafasi nzuri ya kujua idadi ya watu walijitokeza katika muda wa awali kabla haujaongezwa

No comments:

Post a Comment