Ilichanganywa na dawa ya madoa Jik
Wakati
Serikali imeeleza kusikitishwa kwake kufuatia vifo vya watu saba
vilivyotokana na kunywa pombe aina ya gongo, baadhi ya watu
walionusurika wanadai kuwa gongo hiyo ilichanganywa na dawa ya
kutakatisha nguo aina ya 'Jik' pamoja na spiriti ili kuongeza ukali.
Baadhi ya watu wakizungumza na NIPASHE
Jumapili katika eneo Kigogo Mbuyuni jijini Dar es Salaam jana, walidai
pombe hiyo iliyokuwa ikiuzwa na Hekima Lwambano ambaye naye amefariki
baada ya kunywa kinywaji hicho, ilikuwa kali sana na harufu mbaya kiasi
cha wengine kushindwa kunywa.
Ilielezwa imekuwa ni tabia ya wauzaji
wengi wa pombe ya aina hiyo kufanya uchakachuaji wa kuongeza spiriti na
Jik kwa wakati mmoja kwa ajili ya kuongeza ukali kitu ambacho kinaweza
kuwa hatari endapo viwango vya madawa hayo ikiwa kubwa.
Tukio hilo limekuja siku chache baada ya
gazeti hili kutoa taarifa ya uchunguzi ulioelezea kuwepo na utengenezaji
wa pombe hiyo wakitumia malighafi hatari ikiwa pamoja na madawa,
vyakula vilivyoharibika pamoja na nguo zilizotupwa kwenye madampo
mbalimbali.
Watu waliofariki katika tukio hilo ni
Hekima Lwambano, Mzee Kalacha, Harid Hamisi, Methew Mkude maarufu kama
`Banzi', Mohamed said, Antipas Kayanmba na Mohamed.
WALIONUSURIKA WANENA
Wakiongea na gazeti hili baadhi ya watu
walioathirika walisema imekuwa na nguvu za Mungu kunusurika kwa kifo
kwani mara baada ya kunywa pombe hiyo alihisi maumivu makali ya tumbo,
mgongo, kiuno na macho kukosa nguvu ya kuona.
Walisema kuna watu wengi wameathirika na
pombe hiyo lakini kutokana na wengi wao kunywa na kuondoka sehemu
mbalimbali itakuwa sio rahisi kuwatambua.
Mmoja wa walioathirika ambaye alilazwa
Hospitali ya Amana (jina linahifadhiwa) alisema yeye alikuwa na kawaida
ya kunywa gongo kila mara na hata siku ya tukio alifanya hivyo bila
kujua kitu gani kitakachompata.
Aidha mzee Wiilium Msumi (66) ambaye bado
amelazwa hospitalini hapo alisema kwa miaka mingi anakunywa pombe ya
aina hiyo lakini hajapata tatizo la kiafya, kinachomshangaza mara
alipokunywa pombe hiyo alijikuta akibadilika na kusikia maumivu makali.
"lazima watakuwa wameweka kitu, mimi ni
mywaji wa gongo kwa miaka mingi lakini kwa haya yaliyotokea inanitia
wasiwasi," alieleza.
SERIKALI YAAGIZA MSAKO
Naibu waziri wa Wizara ya mambo ya ndani,
Pereira Silima alisema serikali imeagiza jeshi la polisi kuwakamata watu
wote wanaomiliki vibanda vya kuuzia pombe hiyo haramu ili wafikishwe
katika vyombo vya sheria.
Akiongea wakati alipokwenda kuwajulia hali
wafiwa, alisema wananchi washirikiane katika kuwafichua watu wa aina
hiyo kwani wanaweza kusababisha maafa makubwa katika jamii kwa kuuza
pombe ambayo serikali imepiga marufuku.
Alisema bado serikali inasubiri majibu
kutoka kwa mkemia wa serikali, hata hivyo kuna kila dalili kinywaji
hicho kilichakachuliwa kabla ya kufikishwa kwa walaji.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment