Burhani Yakub, Muheza.
WAKAZI
wa Kata ya Misalai Tarafa ya Amani Wilayani hapa, wamependekeza kuwepo
kwa kipengele cha adhabu ya kumwagiwa maji ya baridi na kisha kuchapwa
viboko kwa mbunge atakayesinzia akiwa kwenye kikao bungeni.
Wamependekeza
pia kwamba adhabu hiyo iambatane na kutoruhusiwa kuhudhuria vikao
vitatu mfululizo pamoja na kuzuiwa kugombea tena kipindi kingine mara
muda wake utakapomalizika.
Walitoa
mapendekezo hayo kwa wajumbe wa Tume ya maoni ya marekebisho ya Katiba
ilipofika Kijiji cha Misalai kukusanya maoni ya wananchi wa Tarafa ya
Amani Wilayani Muheza.
Shukrani Said (23) ambaye ni mkulima wa
Kijiji cha Ziarai Kata ya Misarai wilayani hapa alisema kutokana na
baadhi ya wabunge kuonekana mara kwa mara kupitia runinga inayoonyesha
vikao vya Bunge kuonekana wakiwa wamesinzia kuna kila haja ya Katiba
mpya kuwekwa vifungu vitakavyowabana wasilale bungeni.
“Wabunge
hatukuwatuma waende wakalale, matokeo yake zinapitishwa sheria
zinazotubana, tuliwachagua waende wakatuwakilishe, kwa hiyo kuwe na
kipengele cha adahabu ya viboko,” alisema Shukrani na kusisitiza kuwa
adhabu hiyo inavyofanyika ionyeshwe kwenye runinga.
Richard
Lutangilo wa Kijiji cha Bulwa Wilayani hapa alisema pamoja na adhabu ya
viboko, Katiba iongeze kipengele cha kumwagiwa maji kila mbunge
atakayesinzia na kama haitoshi asipewe ruhusa ya kuhudhuria vikao vitatu
mfululizo na pia asiruhusiwe kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo mara
kipindi chake cha miaka mitano kinapomalizika.
“Hili la viboko
likiwekwa kwenye Katiba litaleta umakini wa wabunge wetu kwani tunawaona
inatuhuzunisha sana sisi wapiga kura tunapowaona wakiwa wamelala fofofo
bungeni wakati vikao vikiendelea,” alisema Jackob
Zephania.
Hadi
Mlowe (50) mkazi wa Kijiji cha Mgambo Wilayani hapa alipendekeza umri
wa wagombea wa nafasi ya ubunge uanzie miaka 45 kwa kuwa amebaini
wabunge vijana ndiyo chanzo cha kukosekana kwa nidhamu ndani ya Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Napendekeza
katiba mpya iweke ukomo wa umri wa kuanzia kwa nafasi ya ubunge ili
kuondokana na chombo hiki muhimu kukosekana kwa nidhamu tunasikia jinsi
wabunge vijana wanavyoropoka linaonekana kama ni Bunge
la kihuni,” alisema Mlowe.
Cleopas
Mutabuzi (50) mkulima wa Kijiji cha Misalai alipendekeza madaraka ya
Rais yapunguzwe hasa katika kuteua mawaziri, ambapo alitaka waajiriwe na
Tume ya Utumishi kwa kufuata taaluma zao na siyo
kuchaguliwa kisiasa.
Kadhalika
nafasi ya Spika, naibu Spika na Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania alipendekeza zisitokane na wabunge bali waajiriwe kupitia
Tume ya Utumishi na baadaye majina yao yapitishwe bungeni kwa ajili ya
kupewa baraka na wabunge.
Kamati hiyo ya kupokea maoni ya marekebisho ya Katiba ilikuwa wilayani hapa kwa muda wa siku tatu ambapo
iliendesha mikutano Majengo, Kwafungo, Mkuzi, Misozwe, Amani na
Misalai.
habari kwa hisani ya gazeti la mwananchi
|
No comments:
Post a Comment