Thursday, July 5, 2012

Hali ya Dk Ulimboka yaendela kuimarika

Hali ya Dk. Stephen Ulimboka, aliyepelekwa nchini Afrika Kusini Jumamosi kwa matibabu baada ya kutekwa, kupigwa na kuumizwa na watu wasiojulikana inaendelea vizuri.

Akitoa taarifa juu ya hali ya Dk. Ulimboka, jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Edwin Chitage, alisema kwa sasa hali yake inaendelea vizuri tofauti na awali alipokuwa hapa nchini.

Alisema Dk. Ulimboka, alifika salama na kupokelewa na madaktari, ambapo alianza kupata matibabu ya haraka.

"Kwa mujibu wa taarifa tulizopata leo (jana), hali ya Dk. Ulimboka inaendelea vizuri na bado anaendelea kupatiwa matibabu. Hali yake siyo mbaya sana wala nzuri sana," alisema Dk. Chitage.



Kuhusiana na jina la Hospitali anayotibiwa Dk. Ulimboka huko Afrika ya Kusini, Dk. Chitage, alisema hawezi kutaja kutokana na kuhofia maisha na usalama wa Dk. Ulimboka yatakuwa shakani huko aliko.

“Ndugu mwandishi nadhani unafahamu tukio zima lililompata Dk. Ulimboka, hivyo kutaja hospitali anayotibiwa kwa sasa ni sawa na kumtangazia kifo,” alisema Chitage.

Ni muda wa wiki moja umepita tangu Dk. Ulimboka alipotekwa katika mtaa wa Tunisi, Kinondoni, jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana na baadaye kukutwa katika eneo la msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji hilo, huku akiwa katika hali mbaya na majeraha mwili mzima pasipo kujitambua.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment