Tuesday, July 17, 2012

Kanisa lamkana Kova


  Lataka lisihusishwe, hakutubu kwao
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
Mapya yameibuliwa na Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo Kawe jijini Dar es Salaam kuhusu sakata la kukamatwa kwa raia wa Kenya, Joshua Gitu Mhindi (31) na limekana kuwa mtu huyo alikwenda kutubu kanisani hapo.
Pia limesema mtu huyo baada ya kukamatwa, walinzi wa kanisa hilo walikubaliana na polisi kwamba wamuachie hasa baada ya yeye mwenyewe kueleza kuwa ana matatizo ya akili na hivyo amekuwa na tabia ya kuropoka ropoka hata katika mambo ambayo siyo ya kweli.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, juzi akizungumza na waandishi wa habari, alisema polisi wamemtia mbaroni mtuhumiwa aliyeshiriki kumteka Dk. Ulimboka na kwamba alikwenda katika Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa lengo la kutubu.

Hata hivyo, akizungumza na mamia ya waumini wakati wa ibada ya Jumapili jana, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Josephat Gwajima, alisema taarifa kwamba Mkenya huyo alikwenda kutubu kanisani hapo zimemshangaza sana na kwamba hata kama ni kweli lakini polisi wamefanya kosa kutangaza jambo hilo.
“Nataka nisahihishe kauli ya kwamba alikuwa anataka kutubu, hapana alikuwa anamtafuta mchungaji kiongozi kuonana naye,” alisema Mchungaji Gwajima.
Alisema lazima ifahamike kuwa watu wa Mungu waliookoka hawana utaratibu wa kwenda kumuona mchungaji kutubu isipokuwa ni kwamba utaratibu ni wakati neno la Mungu likiwa linahubiriwa muumini mwenyewe anamuomba Mungu amsamehe.
Mchungaji Gwajima alisema makanisa yote ya watu waliookoka hayana utaratibu wa waumini kutubu kwa wachungaji.
Alisema kwanza kwa tamaduni za kanisani mtu akienda kutubu zile taarifa za toba yake hazitakiwi kutangazwa kwenye vyombo vya habari maana kwa kufanya hivyo itaonekana Kanisa la Ufufuo na Uzima, linatangaza siri za watu wanaokwenda kutubu dhambi zao.
“Mimi ninachokilaani ni kitendo cha polisi kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa mtu huyo alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo wakati huyu mtu hakuja kanisani kutubu alikuja kumtafuta mchungaji kiongozi, hivyo kanisa haliwezi kukubali suala hilo, kama suala hilo limekuja kwa lengo la kutaka kuvuruga kanisa la Ufufuo nalituma lirudi huko lilikotoka,” alisema Gwajima.
Alisema hatua ya Jeshi la Polisi kutangaza kwamba mtu huyo alikwenda kutubu kanisani hapo, kumezua maswali mengi, inawezekana alitumwa aje atengeneze jambo atokee katika kanisa hilo ambalo lina maelfu ya watu ili jambo hilo liweze kusikika kwa haraka.
Alisema jambo la pili ni kwamba inawezekana mtu huyo ni mhalifu anayetembea hapa na hapa kufanya uhalifu lakini pia inawezekana kweli mtu huyo ameyatenda aliyoyasema ya kumteka Dk. Ulimboka.
“Kila mtu anafahamu kuna wingu zito la utata kati ya madaktari na serikali kwa hiyo watu wanaweza kutafsiri kuwa Kanisa la Ufufuo na Uzima limeandaliwa kuisafisha serikali katika jambo hili, hapana sisi hatuwezi kukubali, na uzuri kanisa letu limekuwa mstari wa mbele kusema ukweli daima,” alisema Gwajima.
Alisema Jeshi la Polisi limefanya vizuri kumkamata raia huyo wa Kenya hata kama ni kichaa lakini lazima ifahamike kuwa kama mtu huyo alishiriki kumteka Dk. Ulimboka, suala hilo halilihusu Kanisa la Ufufuo na Uzima na kwamba kanisa halina mashiko kwenye jambo hilo.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi kabla halijafanya lolote kwa raia huyo wa Kenya apimwe akili ili kubaini kama ana akili sawa.

USHAURI WA KANISA KWA JESHI LA POLISI
Mchungaji huyo alisema katika mgogoro wa madaktari na serikali kuna mtu ambaye ametajwa na jamii ni bora akatafutwa na kuhojiwa.
Alisema kuna uwezekano mkubwa Rais Jakaya Kikwete katika jambo hilo alishauriwa vibaya, kwani Rais mwenyewe ameonyesha kuwa na nia njema na suala hilo, ndio maana siku aliyohutubia wananchi alisema kati ya waliotuhumiwa kumteka Dk. Ulimboka serikali ni mmojawapo hivyo ni bora kuwepo uchunguzi huru.

MSIMAMO WA KANISA
Alisema katika mgogoro huo msimamo wa Kanisa la Ufufuo na Uzima ni kuwataka madaktari wasitishe mgomo na kuendelea na kazi ili kuepusha vifo vya watu vinavyotokana na kuwepo kwa mgogoro huo.
Alisema serikali iache ubabe kwani madaktari ni watoto wake hivyo inapaswa kukaa nao kujadiliana suala hilo ili liweze kufikiwa mwafaka.
Mchungaji Gwajima alisema kanisa linamuombea Dk.Ulimboka arejee nchini akiwa salama kutoka huko Afrika Kusini alikopelekwa ili aje asaidie upelelezi pa kuanzia.
ASIMULIA JINSI RAIA HUYO WA KENYA ALIVYOKAMATWA
Alisema kati Juni 26 na 27, mwaka huu kanisa hilo lilifanya maombi kwa ajili Dk. Ulimboka baada ya kuona si jambo zuri kwa daktari kutekwa na pia tulizungumzia suala la na mgomo wa madaktari na kuhoji sababu za serikali kuchelewa kuupatia ufumbuzi.
Alisema baada ya kumaliza maombi hayo alitokea mtu mmoja ambaye aliomba kuonana na Mchungaji Kiongozi na walinzi wa kanisa hilo walimweleza kuwa hawawezi kumruhusu kuonana naye na badala yake wakamtaka aeleze shida yake.
Alisema pamoja na walinzi kushikilia msimamo huo, mtu huyo aling’ang’ania kuwa anataka kumuona mchungaji, jambo lililowashtua hasa kutokana na jinsi mtu huyo alivyokuwa akizungumza na alionekana siyo mtu wa kawaida.
Alisema walinzi walibaini kuwa mtu huyo si salama kwa jinsi alivyokuwa akiongea na walipombana zaidi mtu huyo akasema ametokea Kenya na kwamba yeye ni Mkenya na kwamba ana mambo mengi ya kumweleza mchungaji kuhusu yeye na wenzake wa kikundi cha Gun Star kuhusika kumteka Dk. Ulimboka.
Gwajima alisema walinzi waliposikia maneno hayo waliamua kumpeleka Polisi.
Hata hivyo, walipitia alikokuwa amefikia nyumba ya kulala wageni iliyopo maeno ya Kawe ambako walichukua mikoba yake.
Alisema walipofika Polisi Kawe, walieleza yaliyotokea na kutakiwa wamwache hapo kituoni.
WIKI TATU BAADAYE
Mchungaji Gwajima alisema wiki tatu zilipopita tangu mtu huyo akamatwe Polisi Makao Makuu walipiga simu kanisani kutafuta walinzi waliomkamata raia huyo wa Kenya ambapo walikwenda Mchungaji Joseph Marwa na mtu mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ernest kutoa maelezo.
Alisema walinzi hao baada ya kufika makao makuu polisi mtu huyo aliitwa mbele ya watu hao na kueleza mambo aliyosema kanisani alipokamatwa na yanafanana na aliyowaeleza polisi.
Hata hivyo, mtu huyo alipoulizwa ni kwanini amesema maneno hayo alidai kuwa ana matatizo ya akili na kwamba mapepo yakimwingia kichwani huwa anaropoka maneno hovyo.
“Mtu huyo alisema mbele ya polisi na walinzi wa kanisa hilo kwamba ana matatizo ya kuropoka hata kama maneno hayo hayana ukweli ambapo alipiga magoti mbele ya polisi na walinzi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kuomba asamehewe kwa sababu ana tatizo la kuropoka kusema mambo ambayo hata kama hayapo,” alisema Gwajima.
Alisema katika hali ya kushangaza siku mbili baadaye, aliona kwenye vyombo vya habari Polisi wakitangaza kwamba mtu huyo alikwenda kutubu kwenye kanisa lao.
KAMANDA KOVA AZUNGUMZIA TAMKO LA KANISA
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kova akizungumza na NIPASHE alisema leo ataitisha mkutano wa waandishi wa habari kuelezea mambo mbalimbali na akiulizwa swali linalohusiana na tamko la kanisa hilo atalitolea ufafanuzi.
Kova alisema kimsingi hataki kulumbana na viongozi wa kanisa hilo na kwamba kama ni suala la kwamba mtu huyo alikuwa hana akili kama ilivyoelezwa anayepaswa kuthibitisha hilo ni daktari.
Tangu Dk.Ulimboka atekwe na kuteswa na watu wasiojulika jambo hilo limekuwa na utata kuhusu watu gani waliohusika na tukio hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment