18 watiwa mbaroni, kufikishwa kortini
Mwenyekiti
wa Umoja wa Vijana Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kata ya Ndago Wilaya
Iramba mkoani Singida, Yohana Mpinga (30), ameuawa baada ya kutokea
vurugu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kamanda wa Polisi Mkoa Singida, Kamshina
Msaidizi wa Polisi, Linus Sinzumwa, alisema tukio hilo lilitokea saa
10:00 jioni katika kijiji cha Ndago.
Alisema siku hiyo, Chadema walikuwa na
mkutano wao halali, lakini wakati wakiendelea, kulizuka vurugu kubwa
kati ya wafuasi wa chama hicho na wa CCM.
Kwa mujibu wa Kamanda Sinzumwa, mawe na fimbo zilitumika kwenye vurugu hizo.
Alisema mkutano huo ulikuwa ukihutubiwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, Mwita Waitara na Kitila Mkumbo.
Alisema baada ya vurugu kupamba moto,
marehemu alikimbia hadi kwenye nyumba ya mwalimu Shume Lyanga, lakini
alifuatwa ndani na watu wanaodaiwa kuwa ni wafuasi wa Chadema na
kuadhibiwa hadi kifo.
Watu 18 wametiwa mbaroni kutokana na tukio
hilo na polisi wamesema watachujwa kubaini wahusika halisi ili
wapandishwe kizimbani kujibu tuhuma za mauaji.
Hata hivyo, habari zaidi kutoka eneo la
tukio ambazo zimekanushwa na Kamanda Sinzumwa, zinasema kigogo na
kiongozi mmoja wa CCM aliwakodi vijana kutoka jirani na eneo la mkutano
kwa lengo la kuleta vurugu ili mikutano ya Chadema isifanyike.
Inasemekana kuwa kigogo huyo aliwakodishia gari dogo aina ya Hiace na kuwagharimia malazi, chakula na kuwalewesha kwa pombe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la
Vijana Chadema (Bavicha) Mkoa wa Singida, Joseph Isango, alisema chama
chake hakihusiki na vurugu hizo, kwani eneo la tukio wafuasi wake
walivumilia sana, kabla ya kutokea vurugu.
Wakati huo huo, Chadema imekanusha kuhusika na vurugu hizo.
Ofisa wa Sera na Utafiti wa Chadema,
Waitara Mwikwabe, alisema chama hicho kiliandaa mikutano ya hadhara
katika Jimbo la Iramba Magharibi na kwamba mikutano hiyo ilitolewa
taarifa polisi na mkuu wa polisi kutoa baraka zote kama utaratibu wa
sheria unavyotaka kwa barua yenye kumb. Na KIO/BI/1/VOL.V/268 ya Julai
12, mwaka huu.
Waitara alisema vurugu zilitokea wakati
wakijiandaa kuanza hotuba, ndipo vijana wapatao wanane walianza
chokochoko kwa kutoa lugha ya matusi na punde mawe yakaanza kurushwa
kutoka sehemu mbalimbali.
Alisema hadi wanamaliza mkutano huo
uliokuwa wa amani na utulivu baada ya kuondolewa vijana hao,
wazungumzaji walijenga hoja juu ya mustakabali wa jimbo na taifa kwa
ujumla.
Aliongeza kuwa wananchi waliohudhuria
walitaka viongozi wa Chadema waendelee kuhutubia, lakini walibanwa na
ratiba ya kuwahi mkutano wa pili, Kinampanda.
Hata hivyo, Waitara alisema walitoa
taarifa kituo kidogo cha polisi Ndago kwa kufungua jalada na kupewa RB
namba NDG/RB/190/2012 ambapo waliwataja baadhi vijana waliowatuhumu
kuhusika katika vurugu hizo.
Vijana waliofunguliwa mashitaka katika
kituo hicho ni pamoja na Daniel Sima, Tito Nitwa, Bakili Ayubu, Yohana
Makala Mpande, Ernest Kadege, Simion Makacha, Anthony John na Frank
Yesaya.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment