Tuesday, July 17, 2012

Polisi lafunga mjadala wa aliyemteka Dk Ulimboka


POLISI Kanda Maalum ya Dar es Salaam imesema suala la raia wa Kenya, Joshua Gitu Muhindi (31) anayetuhumiwa kumteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka halizungumziki kwa sababu tayari liko mahakamani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kamanda wa polisi wa kanda hiyo, Suleiman Kova alisema tayari mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani, hivyo kujadili suala hilo ni kuingilia uhuru wa mahakama.
Pia, Kova alisema maelezo kwamba mtuhumiwa ni kichaa, kisheria daktari ndiye mwenye uwezo wa kupima kwani hata kichaa anatawaliwa na sheria.

“Vichaa vina madaraja, mtu mwingine anaweza kuwa na kichaa cha kawaida na mwingine kile kilichoshindikana. Hivyo mahakama ndiyo itaangalia kama wakati alipokuwa anafanya kosa hali aliyokuwa nayo,” alisema Kova na kuongeza:

“Ninachoweza kusema ni kwamba yale yote niliyowaambia Julai 13 (Ijumaa iliyopita) nimeangalia tena katika kumbukumbu za polisi na ndiyo ushahidi wenyewe.”
Kova alisema wao hawawezi kuingia malumbano na taasisi yoyote ya dini,kwani wanaangalia usalama wa raia na mali zao.

“Namheshimu sana Gwajima kwa sababu nawaheshimu viongozi wa dini na hatuwezi kuingia katika mtego wa malumbano na viongozi wa dini, kwa sababu tunafanya kazi kwa pamoja,” alisema.
Pia, alisema taarifa aliyotoa wiki iliyopita ilikuwa ya awali na kwamba, kuna vitu vingi ambavyo vikijulikana wazi vinaweza kuathiri upelelezi au uhuru wa mahakama na kusababisha mshtakiwa au mlalamikaji kukosa haki.

Wiki iliyopita, Kova alisema Muhindi alikamatwa Juni 29, mwaka huu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe, baada ya taarifa kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema raia huyo mwenye kitambulisho cha utaifa namba 29166938 kilichotolewa Oktoba 11, 2010 Wilaya ya Nyeri nchini Kenya, pia anamiliki hati ya dharura ya kusafiria yenye namba 0123431 iliyotolewa Juni 14, mwaka huu Namanga Kenya.

Kwa mujibu wa Kova, baada ya kuhojiwa na polisi, raia huyo alisema alikuja nchini Juni 23, mwaka huu kufanya tukio lililotokea Juni 25, mwaka huu na kwamba alijulishwa kuwa yeye na wenzake 12 ndiyo walipangwa kutekeleza tukio hilo.

Alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kijulikanacho kama Gun Star chenye makao yake Iwiru wilaya ya Thika nchini Kenya na kwamba kinaongozwa na mtu mmoja ajulikanaye kama Silencer akisaidiwa na Paft.

Alisema baada ya utekaji huo, Juni 29 mwaka huu raia huyo alikwenda katika kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe kwa nia ya kutaka kuonana na kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji Gwajima lakini hakufanikiwa badala yake alionana na msaidizi wake ajulikanaye kama Joseph Marwa Kiriba.

No comments:

Post a Comment