Askari wakiwa wamebeba mwili wa mtu
Uchunguzi wa NIPASHE umebaini kwamba kazi ya utafutaji wa maiti ilisitishwa majira ya saa 7:30 mchana baada ya bahari kuchafuka na kusababisha wazamiaji hao kushindwa kufanya kazi yao.
“Tumeamua kusitisha zoezi la kutafuta maiti baada ya bahari kuchafuka na mawimbi makubwa kutokea katika eneo la tukio," alisema mzamiaji Ali Ramadhan.
Hata hivyo, alisema kwamba viongozi ndiyo watatoa maamuzi baadaye kama kazi hiyo itaendelea kufanyika leo au la kwa kuzingatia maendeleo ya hali ya hewa ya baharini huko katika mkondo wa pungume kilomita 12 kutoka bandari ya Malindi.
Hata hivyo, wazamiaji hao walisema pamoja na kujitahidi kuzamia umbali wa kina cha mita 25, meli hiyo haionekani kutokana na kuzama katika mkondo mkubwa wa Bahari ya Hindi.
Ramadhan alisema kwamba juzi walifanikiwa kuona eneo moja likiwa na mafuta mengi ya yakielea juu ya bahari na kuweka alama ya maboya kwa kutumia nanga kwa lengo la kuanzia uchunguzi katika eneo hilo lakini wameshindwa kutokana na bahari kuchafuka jana.
Wazamiaji hao wanatokea kikosi cha wanamaji baharini cha Jeshi la Polisi, Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Jumuiya ya wavuvi wa kojani, pamoja na wazamiaji wa kujitolea Zanzibar.
Daktari msimamizi katika kambi ya kupokea maiti, Dk, Msafiri Marijani alisema kwamba idadi ya maiti zimefikia 68 na hadi jana mchana maiti ilikuwa imebaki moja.
Alisema kwamba kuna maiti ya mzungu mmoja mwanamke bado haijajulikana na imehifadhiwa katika hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar. Aidha alisema kwamba maiti tisa za wanawake wakiwemo watoto wawili zimelazimika kuzikwa jana katika eneo la Kama baada ya kutotambuliwa na ndugu zao.
“Mazishi ya watu hao gharama zake zote zimegharamiwa na serikali,” alisema Dk Marijani.
Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Serikali ya Muungano imetuma madaktari bingwa wanaogonzwa na Dk Patrice Sarafin kuongeza nguvu katika hospitali ya rufaa ya Mnazi Mmoja Zanzibar. Kikosi cha madaktari hao bingwa tayari kimeanza kutoa huduma kwa majeruhi wa meli hiyo ambao wamelazwa katika hospitali hiyo tangu jana.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Zanzibar, Khamis Suleiman, alisema kwamba vyombo vya usafiri wa baharini vimekuwa vikipewa ripoti za mabadiliko ya hali ya hewa kila siku kupitia Ofisi ya bandarini Tanzania bara.
Mkurugenzi wa Huduma za utabiri wa hali ya hewa, Dk. Hamza Kabelwa, alisema kwamba kabla ya meli hiyo kuzama walitoa taarifa kwa vyombo vya usafiri baharini kuhusu kutokea upepo mkali kuanzia saa 2:00 asubuhi ya Julai 17, mwaka huu.
Upepo huo ulikuwa ukivuma kwa kasi ya kilometa tatu kwa saa lakini vyombo siku hiyo viliachiwa na kufanya safari kabla ya meli hiyo kupigwa na mawimbi makali ya bahari na kuzama katika eneo la Pungume Zanzibar.
Hata hivyo, wakizungumza na NIPASHE baadhi ya mabaharia katika Bandari ya Malindi walisema kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu (Sumatra) na Mamlaka ya Usafirishaji baharini Zanzibar (ZMA), zimeshindwa kusimamia taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kwa vyombo vya usafiri nchini.
Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Mkurugenzi wa ZMA, Abdalla Hussen Kombo, alisema kwamba taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa kimsingi hupokelewa na Kituo cha Uokozi na ufuatiliaji baharini na wao ndiyo wenye jukumu la kusimamia utekelezaji wake.
Alisema kwamba kituo hicho ndiyo kinatakiwa kufanya kazi ya kufuatilia matukio yote ya ajali baharini yanapotokea pamoja na kuzuia chombo kusafiri kwa kushirikiana na mamlaka nyingine. Katika mji wa Zanzibar hali imeanza kurejea kawaida ikiwemo baadhi ya barabara zilizokuwa zimefungwa kupisha shughuli za uokozi zimeanza kufunguliwa Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Hamad Masoud Hamad, amesema anazo taarifa kuwa kuna Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW), anatayarisha hoja binafsi ya kumshinikiza kuchukua hatua ya kujiuzulu kufuatia ajali hiyo.
Hata hivyo, alisema kwamba hoja hiyo inatayarishwa kwa chuki binafsi na watu wasiopenda Serikali ya Umoja wa kitaifa na kuendelea kutetea msimamo wake kamwe hatojiuzulu wadhifa huo kwa kuwa ajali hiyo imetokana na mipango ya Mwenyezi Mungu.
Wakati huo huo, kumekuwepo na utata mkubwa kuhusu idadi ya abiria waliyokuwemo katika meli hiyo baada ya Mkurugenzi wa ZMA kueleza mali hiyo iliruhusiwa kubeba abiria mwisho 250 baada ya kukaguliwa na kupewa lesseni ya biashara hiyo.
Hata hivyo, taarifa ya Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kwa vyombo vya habari imesema meli hiyo ilikuwa na abiria 290 na mabaharia tisa wa meli hiyo. Hadi sasa jumla ya maiti 68 zimepatikana na watu 150 wameokolewa ambapo watu 72 awajulikani walipo kufuatia ajali hiyo.
Maiti waliotambuliwa hadi jana ni Halima Ramadhan (58) (Morogoro), Hadija Omar Ally (58) (Kilimahewa), Amina Hamid Bakary (39) (Chukwani), Mwanahamisi Mshauri (42) (Kibandamaiti), Ali Abul Othman (35) (Mkwajuni), Hadija Othman Juma (50) (Bambi) na Mohamed Said Salum (40) (Magomeni).
Wengine Amina Ahmed Ramadhan (21) (Michezani), Asiya Juma Khamis (29) (Kiembesamaki), Yussuf Hassan Yussuf (7) (Chamanzi), Batuli Abdulrahman Ameir (20) (Jang'ombe), Halima Ali Mohamed (35) (Kiwengwa) na Fatma Said Sutan (54) (Msasani) na Mgeni Juma Khalfan (25) (Darajabuvu) Zanzibar.
Wengine Hadija Rajabu Kigune (22) (Fuoni), Maua Ramadhan Feruzi (29), Hussen Ali Khamis (4) (Kwerekwe) na Sabiha Kheir Mbarouk (25) (Mgerema), Kisiwani Pemba.
Maiti wengine ni Riziki Mohammed Iddi (25) (Fuoni), Mwanahamisi Khamis Haji (75) (Jang'ombe), Amina Shaaban Kilenga (24) (Jang'ombe), Raki Victor Kadogo 28 (Mbagala) Damas Leo Mlima (54) (Shangani), Halima Sharif Abdullah (21) (Shangani), Ali Juma Ali (44) (Jang'ombe), Raya Ramadhan Hassan (miezi miwili) (Shakani) Mariam Iddi Omary (25) (Shakani) Mariam Mwanahisha Omary Juma (Bunju) na Usina Ali Khamis (34) (Bagamoyo).
Wengine ni Kursumu Haji Khamisi (25) (Kilimahewa), Sichana Pandu Simai (43) (Chumbuni), Nadra Maulidi (17) (Morogoro), Mwanahidi Abdalla Ramadhan (21) (Meya), Zubeda Jumanne na mtoto wa miezi saba Iddi Masoud Omar (Tomondo) Zanzibar.
MAITI ZAPOKELEWA DAR ES SALAAM
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alisema kuwa jana wamepokea maiti nne kutoka Zanzibar ambazo tayari wameshazisafirishwa kwenda kwa wahusika ili kuendelea na mazishi.
Alisema maiti ya kwanza ambayo ni ya Zainabu Shabani imesafirishwa na kupelekwa katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na nyingine ya Lucky Victor ambayo imepelekwa eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, alisema maiti mbili ambayo ni ya Mwanaidi Abdallah pamoja na ya Halima Ramadhani zimesafirishwa na kupelekwa mkoani Morogoro katika eneo la Kihonda kwa ajili ya mazishi na kwamba maiti hizo mbili ni mtu na ndugu yake.
Alisema maiti hizo walizipokea majira ya saa 3 asubuhi na kupanga utaratibu wa kuzisafirisha muda huo huo katika mikoa hiyo.
Pia alisema wamewapokea watu wawili ambao waliwasafirisha kwa ndege kutoka katika Hospitali ya Mnazi mmoja iliyoko Zanzibar baada ya kupata nafuu na tayari wamepelekwa nyumbani kwao katika eneo la Yombo Kiwalani.
Baadhi ya ndugu jana walijikuta katika wakati mgumu baada ya kujulishwa kuwa maiti ambazo zinasafirishwa kutokea Zanzibar ni zile ambazo tayari zimeshatambuliwa na jamaa zao.
Ndugu wengine walikuwa katika hali ya simanzi wakiwa wanasubiri muda ufike ili waweze kupanda meli na kuelekea Zanzibar kwa lengo la kuwatambua ndugu zao.
Marehemu wote wapumzike kwa amani na mwanga wa milele Mwenyezi Mungu awaangazie na poleni sana ndugu na jamaa mliofikwa janga hili na ni letu sote tuko pamoja.
ReplyDeleteAmina Damson MUNGU wetu ni mwenye huruma muelewa na hutoa haki kwa kila mmoja hakika maombi yako yatafika kama makusudio yako na mungu akutie nguvu wewe, ndugu ,jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu mkubwa wakitaifa
ReplyDelete