Tuesday, August 14, 2012

CCM: Harambee ya Chadema ni usanii

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa madai ya kufanya usanii wa harambee kuhalalisha uwepo wa mabilioni ya fedha zilizotolewa na wafadhili wao kutoka nje ya nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kitendo kinachofanywa na Chadema ni kuwahadaa Watanzania.

Alisema chama hicho kimekuwa kikiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie huku tayari wakiwa wameshapata mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili wao.

"Mfano mzuri ni harambee waliyoifanya katika Hoteli ya Serena baada ya kupewa mabilioni na wafadhili wao ili mradi wahalalishe kuwa pesa wanazozitumia zimetokana na michango ya Watanzania wakati si kweli," alidai Nnauye.

Alidai kuwa CCM ina ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa Chadema wamepewa na wafadhili wao kwa lengo la kuendeleza operesheni mbalimbali nchini.



Aidha, Nnauye alihoji sababu za fedha hizo kutolewa kwa Chadema hivi sasa wakati nchi imeendelea kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwemo gesi na mafuta.

Alisema kama ufadhili huo ni wa nia njema na nchi, basi Chadema inapaswa kuweka wazi masharti ya ufadhili huo ili Watanzania wajue kama una manufaa.

Alisema kama Chadema hawataeleza, basi CCM itawaeleza Watanzania ukweli wa suala hilo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi  Chadema, John Mnyika, akitoa tamko la chama chao juu ya madai hayo ya CCM, alisema ni ukweli ulio wazi kwamba Chadema imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi.

Mnyika alifafanua kuwa michango hiyo imekuwa ikitolewa kwa njia ya simu na inaweza kufuatiliwa na kuthibitishwa bila shaka yoyote.

Alisema michango hiyo inadhihirisha jinsi Watanzania walivyoamua kuchangia mabadiliko ya kweli.

Mnyika alisema madai ya CCM kuwa Chadema imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na kuitaka itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje yanayokifadhili chama hicho.

Alisema kuibuka huko kwa CCM na kufanya propaganda chafu, ni ishara ya kwamba inaumizwa na namna ambavyo Watanzania wanajitokeza kuunga mkono chama chao kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment