Jane Wangui Mbuga, manusura wa ajali ya
barabarani huko Makole, jirani na daraja la Wami mkoa wa Pwani akiwa
amelazwa kwenye Taasisi ya Mifupa MOI.
Jitihada zilizofanywa na Serikali ya Kenya kutuma
helkopta ya jeshi kuwasafirisha majeruhi na maiti wa ajali iliyoua
Wakenya 12 na kujeruhi wengine 72, zimepongezwa ingawa majeruhi Mary
Mungai, alisahaulika wodini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza na NIPASHE Jumapili jana,
Ofisa Habari wa Muhimbili Aminiel Aligaesha, alisema majeruhi hao
walianza kuchukuliwa Ijumaa kati ya saa 2:00 na saa 4:00 usiku na
kwamba safari ya mwisho iliyofanyika saa 4:00 waokoaji hao waliamini
kuwa walikuwa wamemaliza kazi ya kuwapakia na kuwarudisha nyumbani
Nairobi.
Walisafirishwa kwa magari ya wagonjwa kutoka Muhimbili hadi uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam.
Alisema katika heka heka hizo za
kuwachukua wagonjwa, Mungai aliyekuwa amelazwa wodi namba nane
Kibasila alisahaulika na kwamba alirejeshwa nyumbani jana kwa ndege
majira ya mchana baada ya mawasiliano kufanyika.
Alisema hawezi kuelewa sababu za
kusahulika kwa mgonjwa huyo na kuongeza kuwa pengine ni kuchanganyikiwa
kulitokana na ajali hiyo.
Wasafiri 84 wakiwa wanakwaya wa Kanisa la
Presbyterian kutoka Thika nchini Kenya, wakiwa katika safari ya
kuelekea Zanzibar na Dar es Salaam walipata ajali iliyosababisha vifo
vya watu 12 na kujeruhi wengine 72.
Ajali hiyo iliyohusisha magari manne
ilitokea juzi saa 11 alfajiri katika kijiji cha Makole karibu na daraja
la mto Wami, mkoani Pwani na kuua watu 12 na kujeruhi wengine 72.
Kufuatia tukio hilo, Rais wa Kenya Mwai
Kibaki, aliagiza helikopta ya jeshi la nchi hiyo kutua Dar es Salaam na
kuwarudisha nyumbani majeruhi na miili ya wahanga wa ajali hiyo.
Ofisa Habari alisema Muhimbili ilipokea
watu 72, kati yao 14 walikuwa na majeruhi makubwa wakati 58 walikuwa
na majeraha madogo madogo ukiwemo mshtuko na kwamba maiti zilikuwa
12.
Kwa upande wake Msemaji wa Taasisi ya
Mifupa (MOI) , Jumaa Almas, alisema majeruhi Jane Wangui, anaendelea
kupatiwa matibabu hospitalini hapo kutokana na maumivu ya mgongo, ambayo
yalizuia kusafirishwa juzi pamoja na wenzake.
Alieleza kuwa MOI ilipokea wagonjwa 18
ambao waliondoka na kubakiwa na Wangui aliyeumia vibaya sehemu za
mgongoni na kwamba anaendelea vizuri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani ilipotokea
ajali hiyo, Ernest Mangu, alisema katika ajali hiyo iliyohusisha
matukio mawili, mkasa wa kwanza ulikuwa wa gari namba KBQ 203P
iliyokuwa imewabeba waumini hao kuacha njia na kutumbukia shimoni.
Aliliambia gazeti hili kuwa chanzo cha
kuingia shimoni hakijajulikana hadi sasa na kuendelea kusema kuwa ajali
ya pili iliyotokea muda mfupi, ilisababishwa na uzembe wa dereva wa
lori lenye namba T 229 AFP lililokuwa na trela namba T 785 AFX
lililokuwa likitokea Tanga kuelekea Dar es Salaam kuligonga ubavuni
gari la waumini hao lenye namba KBL 044M lililokuwa limesimama
kuwasaidia wenzao waliokuwa wameangukia korongoni.
Alisema dereva huyo ambaye hata hivyo
hakumtaja jina, anashilikia na polisi akisubiri kufunguliwa mashtaka na
pia uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
Vyombo vya habari nchini Kenya viliikariri
polisi kuwa zaidi ya waumini 80 waliokuwa kwenye mabasi mawili madogo
walikuwa wakielekea Dar es Salaam na Zanzibar kwa ajili ya shuguli zao
za kidini.
Wakati huo huo, kutoka Nairobi nchini
Kenya , Wakenya wamejitokeza kwenye mitandao kutoa maoni ya kumpongeza
Rais Mwai Kibaki kwa hatua ya kuagiza helkopta ya Jeshi la Kenya
kuwafuata na kuwarudisha nyumbani mara moja majeruhi na miili ya
marehemu waliojeruhiwa na kupoteza maisha katika ajali hiyo.
Walimpongeza Rais wao kwa kufanya maamuzi
ya kutuma helkopta ili kuwapeleka Nairobi kwa matibabu na mazishi
kwa kutumia mtandao wa gazeti la kila siku la the Daily Nation na hizi
ni baadhi ya taarifa za ujumbe mfupi walizomtumia;
“Hivi ndivyo Mkuu wa nchi anayejali
anavyowafanyia raia wake” “ Huyu ni Rais mwenye utu ameonyesha
majukumu yake kwa Wakenya walioko hata nje ya mipaka . Haya ndiyo
yanayoufanya uongozi ulioheshimika. Rais wa kwanza anayejali Wakenya na
mambo mengine yanayowakuta hata wakiwa nje ya mipaka yao.”
“Maagizo mazuri mheshimiwa Rais amefanya,” “Hii inaonyesha jinsi anavyowajali wananchi wake Mungu azidi kuwa naye”
“Namheshimu Rais kwa kuchukua maamuzi
magumu na hatua za kuwasaidia majeruhi na kusaidia familia zao na za
wafiwa hiki ndicho serikali ya watu inachotakiwa kukifanya . Maisha ya
Mkenya aliyeko mbali yanatakiwa kulindwa kama ya Wakenya milioni 40. Hii
ndiyo serikali ya kidemokrasia na inayowajibika kwa watu wake .
Haijalishi chochote lakini lifanyike lolote ili kuokoa maisha ya raia
wake.”
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment