Wednesday, September 19, 2012

Jina la Nape latumika kutapeli wagombea CCM



Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
Waandishi Wetu
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema kumezuka mchezo mchafu katika mbio za uchaguzi wa ndani wa chama hicho zinazoelekea ukingoni, baada ya baadhi ya watu kutumia jina lake kuomba rushwa kutoka kwa wagombea ili wawapitishe katika vikao vinavyoendelea mjini Dodoma.

Baada ya kuanza kwa uchaguzi huo Machi mwaka huu, CCM sasa kimeanza vikao vya ngazi ya kitaifa kwa ajili ya kuteua majina ya wagombea wa ngazi za mikoa na taifa. Juzi, kikao cha Sekretarieti ya chama hicho kilianza kufanya maandalizi ya vikao vingine viwili, kabla ya Nec inayotarajiwa kufanyika Septemba 25 kuchagua majina ya wagombea hao.

Vikao vitakavyofuata baada ya Sekretarieti ni Kamati ya Maadili, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya CCM (Nec).

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Nape alisema baadhi ya watu wanatumia jina lake kuwatapeli wagombea wakiahidi kuwa watawasaidia wateuliwe katika nafasi mbalimbali walizoomba.
“Kuna mtu anatumia jina langu, anawapigia watu simu na kuwatapeli fedha kwa kisingizio kuwa majina yao yatateuliwa. Nasema huo ni utapeli na waliotoa wajue kuwa wametapeliwa,’’ alisema Nape.

Nape alieleza kuwa mtu huyo amesajili namba kwa jina lake isipokuwa katika jina la pili ameweka herufi N moja badala ya mbili kama ilivyo Nnauye.
Nape alisema baada ya kugundua utapeli huo alitoa taarifa kwenye vyombo vya usalama ili kumfuatilia mtu huyo na kumkamata.

Nape aliwataka wagombea hao kuvuta subira badala ya kukubali kutapeliwa akisema, vikao vinavyoendelea sasa vitateua wagombea safi, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu atakayeteuliwa kwa sababu ya rushwa au ushawishi mwingine wowote.

“Nawatahadharisha kuwa, hakuna na haitawezekana kurudisha jina la mtu yeyote kwa sababu ya rushwa, umaarufu au lobbying (ushawishi) kwa wajumbe,” alisema:

“Kitakachomfanya mtu afurahie kurudishwa kwa jina lake ni uadilifu na sifa njema ndani ya chama na kwa maana hiyo naomba kila mwanachama kuwa mvumilivu na kusubiri matokeo.’’

Katibu huyo alisema mchakato huo utafanywa kwa umakini kuliko vitu vingine na watatumia kila namna kupata vyanzo halisi vya historia ya mtu ili kujiridhisha kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho katika uteuzi.

“Tutatumia kila chanzo halisi kupata habari ya historia ya mtu pamoja na namna ambavyo chama kinamfahamu mtu huyo katika maeneo yake. Pamoja na hayo, tutakuwa makini na mtu huyo kwa mambo kadhaa ambayo tutaamini kuwa hayatakuwa na shaka juu ya uadilifu wake,’’ alisema.

Alisema majina ya wagombea wote kwa ngazi za mikoa na wilaya yanatarajiwa kutangazwa Septemba 25, mwaka huu mara baada ya kukamilika kwa michakato yote.Alisema siku hiyo Halmashauri Kuu ya CCM itamaliza kikao chake mjini Dodoma na majina yatatangazwa siku hiyohiyo ikiwemo ratiba ya uchaguzi wenyewe.

Vijana matumbo joto
Baadhi ya wagombea vijana walioomba nafasi za uongozi Wilaya ya Kahama, Shinyanga wameanza kuingiwa na hofu ya kukatwa majina yao.

Hofu hiyo imetanda baada ya kuona wagombea wenzao wameanza kufanya kampeni akiwemo ndugu wa mmoja wa mawaziri.
Mmoja wa wagombea hao vijana, Robert Kapera ambaye kipindi kilichopita alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya amedai kuwa anashangazwa kuona wenzake wanafanya kampeni kabla ya uteuzi hali ambayo alidai kuwa inawezekana wakawa na siri ya uteuzi wa majina yao.

Kapera anayetaka kupitishwa kugombea nafasi ya ujumbe wa Nec Wilaya ya Kahama alisema hali inakatisha tamaa na kwamba kama haitadhibitiwa, mwenendo wa chama hicho siku zijazo utakuwa mbaya.

Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama, Michael Bundalla amewaonya wagombea wanaoanza kampeni kabla ya uteuzi akisema kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.

Shinyanga hofu tupu
Baadhi ya wanachama wa CCM mjini Shinyanga wameeneza uvumi kwamba Mwenyekiti wa sasa wa Mkoa, Khamis Mgeja ameenguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Taarifa za Mgeja kutoswa kwenye uchaguzi huo zimeelezwa kupangwa na vigogo hao kwa lengo la kupanga safu ya viongozi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.Imedaiwa kwamba mkakati wa kumwengua unaungwa mkono na baadhi ya wabunge ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa hawamuungi mkono.

Habari hii imeandikwa na Habel Chidawali, Dodoma; Shija Felician, Kahama na Mustapha Kapalata, Nzega.(habari kwa hisani ya gazeti la mwananchi)
  

No comments:

Post a Comment