Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa,Othman Rashid
NI KUHUSU TUHUMA ZA MKE WA KIGOGO KUTAPELI, MKURUGENZI AMTAKA IGP KUCHUKUA HATUA, MTUHUMIWA AJITETEA Waandishi Wetu SAKATA
la mke wa kigogo wa polisi kudaiwa kuwatapeli vijana 120 kwa
kuwachangisha zaidi ya Sh100 milioni ili awatafutie kazi Idara ya
Usalama wa Taifa na Takukuru limechukua sura mpya, baada ya Mkurugenzi
wa Usalama wa Taifa, Othman Rashid kuwataka polisi wamkamate na
kumchukulia hatua za kisheria mwanamke huyo.Utapeli huo wa aina
yake, unadaiwa kufanywa na mama huyo kwa kushirikiana na mwanaye (majina
tunayo). Pia yumo kijana anayejulikana zaidi kwa jina moja la Baraka
ambaye kwenye mpango huo, anajitambulisha kuwa anafanya kazi Ikulu.
Akizungumza
na mwandishi wetu Dar es Salaam juzi, Rashid alisema tayari
amewasiliana na Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema kuhusu tuhuma hizo ili
kujua hatua zilizochukuliwa dhidi yake. “Nimewasiliana na IGP Mwema
ili aweze kunipa ufafanuzi kuhusu mke wa kigogo huyo, lakini nashukuru
amenipa ushirikiano na kuniambia kuwa suala hilo wanalishughulikia
kisheria zaidi. Watanipa taarifa pindi watakapokuwa wamekamilisha,”
alisema Rashid.
Alisema huo ni mfano tu wa baadhi ya watu
wanaotumia jina la Usalama wa Taifa kufanya utapeli na kwamba tabia hiyo
tayari imewaingiza baadhi ya watu matatani baada ya kukamatwa na
kuchukuliwa hatua za kisheria na wengine bado wanatafutwa.
Alisema
sheria ni msumeno, hivyo ikibainika mwanamke huyo alijihusisha kutapeli
kwa kutimia jina la Usalama wa Taifa, hatua kali zitachukuliwa dhidi
yake ili iwe fundisho kwa wengine ambao wanatumia majina ya waume zao
kutapeli watu.
Rashid alisema bado ana imani kwamba polisi
itamchukulia hatua za kisheria mwanamke huyo ikiwa itathibitika kwamba
amejihusisha na utapeli kwa kuwa jeshi hilo lipo kulinda usalama wa raia
na mali zao.
Azungumzia tuhuma Akizungumzia madai hayo jana
kigogo huyo wa polisi ambaye mkewe ndiye anayetuhumiwa (jina
tunalihifadhi), alisema tangu mwanzo alielewa kwamba anayezungumziwa ni
mkewe, lakini akakanusha kuhusika katika utapeli huo. Alisema
kutokana na taarifa ambazo zimekuwa zikiandikwa katika gazeti hili na
kumtaja Baraka, vijana wengi waliotapeliwa kutoka mikoa mbalimbali
walifunguka akili zao na kubaini kuwa aliyetajwa katika habari ndiye
aliyekuwa akichukua fedha kwao.
“Jambo linalonisikitisha ni
kwamba, aliyewaletea taarifa hizo za uongo zinazomhusisha mke wangu na
utapeli huu ndiye tapeli aliyekuwa akizunguka mikoa mingi nchini
kutapeli watu. Hata mke wangu ni mmoja wa waliotapeliwa. Alikusudia
kuwapeleka wanafamilia watatu akiwemo mtoto wake, mke wa kaka yake na
wifi yake ambaye tunamlea,” alisema.
Alisema mkewe alitoa fedha
taslimu zisizopungua Sh1.5 milioni, mbali na gharama za kununua bidhaa
na vifaa mbalimbali ambavyo wanafamilia hao wangetakiwa kwenda navyo
mafunzoni. Alisema walishtuka kuwapo dalili za utapeli baada ya watu
waliokuwa wakidai kushughulikia ‘mipango’ hiyo kuanza kutoa ahadi
zisizotekelezwa, huku wakati mwingine simu zao zikipatikana kwa nadra.
Alipotakiwa
kuwataja kwa majina waliokuwa wakishughulikia mipango, ambao walichukua
fedha kutoka kwa mkewe kigogo huyo alisema hakumbuki vizuri majina yao.
Hata hivyo, alisema mmoja wao anaitwa Baraka. Mke wa kigogo huyo
alikataa kuzungumzia tuhuma hizo akisema: “Hayo yote yapo kwa wakubwa,
mimi siwezi kuongelea kitu kilicho ngazi za juu yangu.”
Alipoambiwa
kuwa mwandishi wetu amezungumza na mumewe ambaye ameeleza kuwa mama
huyo naye ni miongoni mwa waathirika katika utapeli huo, hivyo atoe
ufafanuzi alikataa pia kuzungumzia hilo na kukata simu. Mkurugenzi wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah
alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo alisema: “Kwa sasa niko huku Maputo
(Msumbiji), siwezi kuzungumzia suala hilo lakini nikirudi nitafutane
nitatoa ufafanuzi.”
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Polisi
(DCI), Robert Manumba hakutaka kuzungumzia tuhuma hizo akielekeza
atafutwe msemaji wa polisi ambaye simu yake haikupatikana kutwa nzima
jana.
Ilivyokuwa Wiki iliyopita gazeti hili liliripoti habari
kuhusu mke wa kigogo kuwatapeli vijana 120 kwa ahadi ya kuwapa ajira
katika Idara ya Usalama wa Taifa na Takukuru.
Kati ya Agosti 5 na
7, mwaka huu vijana hao 120 kwa nyakati tofauti walipata taarifa kwamba
kuna nafasi za kazi Idara ya Usalama wa Taifa na Takukuru na kwamba
nafasi hizo zinapatikana kupitia kwa vigogo wa vyombo vya ulinzi na
usalama nchini.
Kwa kupitia kwa mtoto wa mwanamke huyo na kupewa
taarifa na rafiki zao, inadaiwa kwamba watu hao ambao wengi wao ni wenye
elimu ya chuo kikuu walielezwa kwamba ili kupata kazi hizo ni lazima
watoe fedha kati ya Sh700,000 hadi Sh1 milioni.
Walielezwa kuwa
mafunzo ya kazi hizo yatatolewa kwa miezi minne katika vyuo vya Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), vilivyopo eneo la Mbweni (Dar es Salaam),
Zanzibar na Monduli (Arusha).
Siku ya kwanza ambayo waliambiwa
kukutana katika viwanja vinavyozunguka uwanja wa zamani wa Taifa, karibu
na Ofisi za Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ili wapelekwe Mbweni kwa
ajili ya kupangiwa vituo vyao vya kazi walielezwa kwamba baadhi yao
majina yao yalikuwa hayajaingizwa katika mfumo. Baada ya wiki moja
walitakiwa kukutana tena eneo hilo ili kupelekwa, lakini walielezwa kuwa
wangepelekwa Septemba 2, mwaka huu kwa kuwa baadhi yao hawakuwa na
namba.
Ilipofika Septemba 2, vijana hao wakati wakielekea Mbweni,
walielezwa kuwa muda umekwenda na hawataweza kupokewa katika kambi hiyo
hivyo kupangishiwa nyumba za kulala wageni zilizopo Tegeta. Hadi
walipofika katika Ofisi za Mwananchi, Ijumaa wiki iliyopita, bado baadhi
yao walikuwa wanaishi katika nyumba hizo na wengine kupewa nauli ili
warudi katika mikoa waliyotoka kwa maelezo kuwa nafasi zitatangazwa
gazetini Oktoba 3, mwaka huu.
Habari zilizolifikia gazeti hili
zimeeleza kuwa polisi imefungua jalada kuhusu tuhuma hizo na tayari
limewahoji watu kadhaa Dar es Salaam na mikoani, lakini mke wa kigogo
huyo hajahojiwa. |
No comments:
Post a Comment