Wednesday, September 19, 2012

Romney ateleza katika kampeni yake ya urais wa Marekani

 Mitt Romney mgombea wa urais wa chama cha Republican
Mgombea wa urais Mitt Romney,anajaribu kujikinga na mshangao kuhusu kampeni yake baada ya Video kumuonesha anawaambia wafadhili wake asilimia 47 ya Wamarekani ni wahanga walio na haki ya kusaidiwa na serikali. 

Mitt Romney hajaomba radhi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu tamko hilo, lakini alikiri kwamba maneno hayo hayajatowa kwa njia ya usanifu na kwamba yalimtoka tu mdomoni.


Mgombea huyo wa chama cha Republican katika uchaguzi wa urais alisema matamshi alioyatoa yanaonesha tofauti baina ya fikra ya Rais Barack Obama ya kuwa na jamii inayosaidiwa na serikali na ile imani yake yeye Romney ya kuwa na msimamo wa kutegemea masoko huru.

 Kampeni ya Rais Obama inajikita juu ya Video hiyo na inaitumia kuwashajaisha wafuasi wa rais wachangie fedha katika juhudu za kumwezesha achaguliwe tena. Lakini leo wasaidizi wa Mitt Romney walikuwa na kibarua kikubwa, wakiwa mbioni kupunguza uharibifu uliosababishwa na matamshi hayo yaliorikodiwa bila ya ruhusa, akiwaambia wafadhili wake kwamba nusu ya Wamarekani wote hawalipi kodi na anaamini kwamba hao ni wahanga.

Idadi ya wanaoitegemea serikali inazidi
Mwaka mmoja uliopita, Mitt Romney, aliye gavana wa zamani wa Mkoa wa Massachusetts, alisema ana wasiwasi na idadi ya watu wanaozidi ambao wanaitegemea serikali ya shirikisho, wakiwemo watu wengi sana ambao wanatagemea kulipiwa na serikali kwa vyakula vyao, moja ya sita ya Wamarekani wakiwa katika umaskini, na Wamarekani milioni 23 wakihangaika kutafuta ajira.

Wachunguzi wa mambo wanasema hali hii iliochomoza inaweza kuwa ni pigo kubwa kwa Mitt Romney ambaye ametajwa na wapinzani wake wa kisiasa kwamba anatetea maslahi ya matajiri.

Video hiyo inasemekana kwamba ilirikodiwa katika tamasha la faragha la kukusanya michango kwa ajili ya Romney. Katika tamasha hilo, Mitt Romney alinukuliwa akisema pindi atachaguliwa kuwa rais, basi uchumi wa Marekani utapigwa jeki na nguvu ya masoko. Mlolongo wa uchunguzi wa maoni ya watu wiki iliopita umeonesha kwamba Rais Obama amempita Mitt Romney katika kuungwa mkono na wananchi katika ngazi ya kitaifa na katika mikoa kadhaa ambako hapo kabla walikuwa wanapishana chupuchupu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu


Wakati huohuo, katika kamepni hiyo ya uchaguzi wa Marekani kumetolewa malalamiko kwamba waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anajiingiza sana katika kampeni hiyo kwa kumpigia debe Mitt Romney.

Itakumbukwa kwamba Netanyahu ni rafiki wa kibinafsi wa Mitt Romney, na watu hao wawili wanakubaliana sana katika masuala ya uhusiano baina ya Marekani na Israel. Licha ya hayo, Benjamin Netanyahu amekuwa akizidi kupinga namna Rais Obama anavolishughulikia suala la kitisho cha nyukliya kutokea Iran.

Wahakiki wa huko Israel wanasema Benjamin Netanyahu amekwenda mbali mno katika kumuunga mkono Mitt Romney, na gazeti la Yediot Aharonot la huko Israel liliuliza: jee Obama ataiadhibu Israel pindi atachaguliwa tena Novemba 6?

Hata hivyo Netanyahu mwenyewe alisema yeye ataendelea kuitaka Marekani iweke wazi mistari miekundu kwamba Iran haitaruhusiwa kuivuka katika programu yake ya kinyukliya.

No comments:

Post a Comment