Maelfu ya wananchi wameandamana kwenye mji mkubwa wa Pakistan, kwa ajili ya kumuombea afya njema msichana mwenye umri wa miaka 14 alijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi na kundi la Taliban katika harakati zake za kupigania haki za wasichana kupata elimu na kulikosoa kundi hilo lenye itikadi kali za Kiislamu.
Maandamano hayo katika mji wa kusini wa Karachi yalikuwa ni makubwa zaidi kufanyika tangu Malala Yousufzai na wanafunzi wenzake wawili walipopigwa risasi Oktoba 9 mwaka huu wakati wakirejea nyumbani kutoka shule.
Maandamano hayo yameandaliwa na chama chenye nguvu kisiasa cha Karachi cha Muttahida Quami. Kiongozi wa chama hicho, Altaf Hussain, aliwahutubia waandamanaji hao kwa njia ya simu kutoka London, Uingereza ambako anaishi uhamishoni, na kuwaita wapiganaji wa Taliban kuwa ni wanyama.
Waandamanaji hao walikuwa wamebeba picha ya Malala na mabango ya kumpongeza kwa ushujaa wake.
No comments:
Post a Comment