Wednesday, October 17, 2012

Mwanamuziku hatiani kwa mauaji A.Kusini


Molemo "Jub Jub" Maarohanye
Mwanamuziki wa kizazi kipya nchini Afrika Kusini Molemo "Jub Jub" Maarohanye amepatikana na hatia ya mauaji na kosa lengine la jaribio la mauaji baada ya kuwagonga kwa gari lake wanafunzi wa shule mnamo mwaka 2010.
Hakimu aliyetoa uamuzi huo, Brian Nemavhidi pia alimpata Maarohanye na hatia ya kuendesha gari kwa kasi na akiwa ametumia madawa ya kulevya.
Maarohanye aliwagonga wanafunzi kwa gari kake mjini Soweto mwaka 2010 na kuwaua wanafunzi wanne huku akiwajeruhi wengine wengi.
Jamaa za watoto waliofariki, walilia wakati jaji akitoa uamuzi wake.
Maarohanye alikuwa mmoja wa wanamuziki wenye sifa sana nchini Afrika Kusini ingawa baada ya kitendo chake umaarufu wake ukaanza kudidimia.
''Tunawapongeza sana viongozi wa mashtaka kwa kuchukua msimamo wa kuwapata na hatia ya mauaji madereva walioendesha magari wakiwa walevi,'' alisema afisaa katika wizara ya sheria.
Mshtakiwa mwenza wa Maarohanye, Themba Tshabalala, pia alihukumiwa kwa kosa la mauaji.
Walikuwa wanatumia madawa ya kulevya wakati magari yao yalipowagonga wanafunzi. Hata hivyo walikana mashtaka dhidi yao.

Wawili hao walikuwa nje kwa dhamana tangu mwaka 2010 mwezi Machi, uamuzi ambao ulisababisha maandamano makubwa ya wanafunzi waliotaka wawili hao kufungwa jela.
Hakimu Nemavhidi, alibatilisha uamuzi wa kuwaachilia kwa dhamana na kuwaweka rumande hadi hukumu itakapotolewa mwezi Novemba tarehe 30

No comments:

Post a Comment