Monday, March 25, 2013
Maandamano ya CCM, Chadema ‘yapigwa stop’
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberetus SabasKamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberetus Sabas
JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha limepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yafanywe na vyama vya CCM na Chadema Machi 25, mwaka huu, ambayo yangefuatiwa na mikutano ya hadhara na kuvitaka vyama hivyo na wafuasi wake kutii sheria bila shuruti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amesema kuwa lengo la maandamano hayo kwa Chadema ni kushinikiza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Naibu wake Philipo Mulugo wajiuzulu, kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka jana.
Alisema vyama hivyo viliomba kufanya maandamano na mikutano ya hadhara siku hiyo hiyo huku CCM ikiomba kufanya maandamano na mkutano wa hadhara kupinga maandamano ya Chadema ya siku hiyo.
Kamanda Sabas, alisema maandamano na mikutano ya vyama hivyo yamesitishwa kwa sababu tayari Serikali imeshaunda Tume kuchunguza kiini cha matokeo hayo mabaya ya kidato cha nne hivyo yakiruhusiwa itakuwa ni kuingilia Tume.
Alisema kuwa katika maombi yao ya kufanya maandamano vyama hivyo viliainisha barabara za kupitia ambazo zilikuwa ni zile zile na hivyo kama wangelikutana kutokana na kutumia barabara hizo kungelitokea vurugu.
Alisema CCM kilikuwa kimepanga kufanya mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, huku Chadema wakipanga kufanya mkutano wa hadhara viwanja vilivyoko karibu na Soko la Kilombero.
Alisema kuwa maandamano hayo yanaweza kuleta uvunjifu wa amani kwa sababu vyama vyote vinapingana katika maandamano yao.
habari kwa hisani ya habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment