Monday, March 25, 2013

WAKILI MAWALLA WA ARUSHA AFARIKI




Giza limeukumba Mkoa wa Arusha baada ya kutokea vifo vya ghafla vya watu maarufu. Jana Wakili Nyaga Mawalla alifariki baada ya kujirusha kutoka ghorofani akiwa jijini Nairobi, Kenya alikokwenda kwa matibabu.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Nyaga alikufa baada ya kujirusha kutoka katika jengo la ghorofa ya hospitali aliyokuwa akitibiwa jijini Nairobi usiku wa kuamkia jana.

Mfanyakazi wa Kampuni ya Mawalla Advocate, John Minja aliliambia wanahabari kuwqa kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kurejeshwa nchini jana.

“Hali yake haikuwa mbaya, kwani juzi mchana tulizungumza naye tukitaka kwenda kumsalimia lakini, alitueleza kuwa angerejea jana nchini,”alisema Minja.


Hata hivyo, bado haijajulikana sababu za kujiua, lakini baadhi ya ndugu zake wanasema ni kutokana na msongo wa mawazo.

Taarifa za kifo cha Mawalla anayemiliki kampuni kadhaa ikiwamo Kampuni ya uwakili ya Mawalla Advocates, kimeshtua wengi akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema taifa limepoteza kijana mwenye maono, akili na mjasiriamali aliyetajirika bila kuiba.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Nyaga. Licha ya udogo wake kiumri, lakini alikuwa mshauri wangu kwenye mambo mengi kiuchumi, kibiashara na kijamii. Nyaga alikuwa kiongozi wa jamii asiye na mipaka katika huduma tofauti na wafanyabiashara wengi nchini walishirikiana naye,” alisema Mbowe.

Mawalla ambaye ni mtoto wa wakili wa kwanza wa kujitegemea nchini, Juma Mawalla alikuwa jijini Nairobi kwa matibabu ya kupungaza sumu mwilini kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za shinikizo la damu kwa muda mrefu.

Wakati kifo hicho cha ghafla cha Mawalla kikitokea, Jiji la Arusha pia linaomboleza kifo kingine cha ghafla cha mfanyabiashara maarufu wa madini, Henry Nyiti kilichotokea mkoani Morogoro.

Nyiti ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Interstate yenye makao yake makuu eneo la Tengeru, wilayani Arumeru alifariki usiku wa kuamkia juzi akiwa Mahenge alikokwenda kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake eneo la Akheri, Arumeru keshokutwa Jumanne.

Akimzungumzia wakili Mawalla, Mbowe alisema mchango wake kwa maendeleo ya jamii hautasahaulika hasa kutokana na kujitolea kuendeleza taaluma ya uwakili kwa kudhamini tuzo ya wakili kijana kwa kutoa dola 5,000 kila mwaka kumsomesha mshindi wa tuzo hiyo.

Mbowe ambaye mwezi uliopita alipokea hati ya kiwanja chenye thamani ya Sh500 milioni iliyotolewa kwa Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na wakili huyo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, alipendekeza hospitali hiyo iitwe Nyaga Mawalla Memorial Hospital kama njia ya kumuenzi.


habari kwa hisani ya father kidevu blog

No comments:

Post a Comment