Thursday, June 8, 2017

MAHAKIMU NCHINI WAKUMBUSHWA JUU YA UFANYAJI KAZI KWA WELEDI NA UADILIFU

MAH1
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali akisisitiza jambo alipokuwa akiongea na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya kukamilisha ukaguzi katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya zilizopo mkoani humo.
MAH2
Mhe. Jaji Mfawidhi akiongea jambo huku akiwaonyesha baadhi ya Mahakimu (hawapo pichani) nakala ya kitabu cha Muongozo wa kufanya ukaguzi wa Mahakama alipokuwa akiongea nao mara baada ya kukamilisha ziara yake ya kukagua, Mahakama za Mwanzo na Wilaya- Njombe.
MAH3
Baadhi ya Waheshimiwa Mahakimu. Waliohudhuria katika kikao kati ya Mhe. Jaji Mfawidhi na Mahakimu Mkoani Njombe.
MAH4
Mahakimu wakiandika baadhi ya masuala muhimu aliongelea Mhe. Jaji Mfawidhi katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mahakama ya Wilaya-Njombe mapema Juni 8.
MAH5MAH6
Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo, ambaye pia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto akiendelea na kazi, Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo yupo Njombe akiendelea na vikao maalum vya kuondosha mlundika wa mashauri linaloendelea kwa sasa.
MAH7
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo-Lupembe iliyopo mkoani Njombe, Mhe. Godfrey Msemwa akiuliza swali ili kupata ufafanuzi
MAH8
Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Agatha Chugulu akitoa ufafanuzi juu ya maswali kadhaa yaliyoulizwa katika kikao hicho.
MAH9
Naibu Msajili, Mhe. Chugulu akiendelea kutoa ufafanuzi
MAH10
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe mara baada ya kika, wa tatu kushoto ni Naibu Msajili, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Agatha Chugulu
MAH11
Muonekano wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi-Njombe, jengo hili limegawanyika sehemu mbili (2), ambapo upande mwingine ipo Mahakama ya Wilaya- Njombe.
MAH12
Muonekano wa sehemu ya jengo la Mahakama ya Wilaya-Njombe (Picha na Mary Gwera, Mahakama)
……………………………………………………………………………………..
Na Mary Gwera, Mahakama, Njombe
JAJI Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Mary Shangali ametoa wito kwa Mahakimu na wadau wa Mahakama nchini kushirikiana kwa pamoja katika kutoa huduma ya haki kwa wananchi.
Aliyasema hayo mapema Juni 07, alipokuwa akiongea na Mahakimu wa Mahakama mkoani Njombe baada ya kuhitimisha ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama katika Mahakama za Mwanzo na Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete pamoja na Gereza la Ludewa na Makete.
“Ushirikiano wa karibu na Wadau wa Mahakama kama Polisi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawakili na Watumishi wa Mahakama n.k  ni muhimu katika kutekeleza shughuli yetu ya utoaji haki kwa wananchi, jambo hili lina faida nyingi mojawapo ikiwa ni kusaidia kupunguza mlundikano wa kesi katika Mahakama zetu,” alifafanua Mhe. Shangali ambaye pia ni Jaji namba moja (1) wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Kwa upange mwingine, Mhe. Jaji Shangali alibainisha changamoto alizokumbana nazo katika ziara yake ya kukagua shughuli za Mahakama mkoani Njombe kuwa ni tatizo kubwa la usafiri wa kuwachukua Mahabusu kutoka Magerezani na kuwarudisha.
“Hii ni moja ya changamoto kubwa niliyokumbana nayo katika Mahakama zote nilizozitembelea mkoani Njombe, changamoto hii haiihusu Mahakama moja kwa moja ipo chini ya Jeshi la Polisi, lakini kwa kuwa tunafanya kazi kwa kutegemeana changamoto hii inatuathiri na inaweza kusababisha mlundikano wa mashauri na Mahabusu magerezani kutokana na Wahusika wa kesi kutofikishwa Mahakamani kwa ajili ya kusikiliza kesi zao kwa wakati stahiki,” alisema Jaji Shangali.
Aliongeza kuwa, katika ziara hiyo malalamiko mengine yaliyotolewa yaliwahusisha baadhi ya Mahakimu kuwa na tabia ya kutowasikiliza Washitakiwa kwa makini na hatimaye kutoa maamuzi tofauti na uhalisia wa shauri husika.
“Naomba niwaombe ninyi Mahakimu mliopo hapa na baadhi ya Mahakimu nchini kutekeleza jukumu la utoaji haki kwa Weledi, kwani Mahakama ndio kimbilio la wananchi hivyo ni vyema kutoa nafasi kusikiliza kwa makini na usahihi pande zote ili kufanya maamuzi yanayostahili,” alieleza Jaji Mfawidhi huyo.
Aidha; Mhe. Jaji Shangali amesisitiza juu ya utoaji wa Adhabu Mbadala kwa watuhumiwa wenye makosa madogo madogo ili kuepuka mlundikano usio wa lazima magerezani.
Akiongelea juu ya Programu maalum ya kuondosha mlundikano wa Mashauri linaloendelea nchini, Jaji Mfawidhi alisema kwa sasa Mahakama kanda ya Iringa inaendelea na kikao maalum cha Mahakama (special session) cha awamu ya tatu (3) kilichoanza rasmi Mei 29 kinachofanyika Njombe chini ya Mhe. Paul Kihwelo ambapo katika kikao hicho jumla ya mashauri 32 yatasikilizwa na kutolewa maamuzi.
“Kikao cha awamu ya kwanza kilianza rasmi Aprili, 24 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa na Makao makuu na kumalizika Mei, 26 mwaka huu, katika kikao hicho jumla ya mashauri 41 yalipangwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi, hata hivyo hadi kufikia Mei 26, jumla ya mashauri 37 yalimalizika huku mengine yakiwa yanaendelea na usikilizwaji wa awali na mengine yakiwa katika hatua ya mwisho ya kutolewa maamuzi,” alisema Jaji Shangali.
Aliongeza kuwa kikao kingine cha pili kilifanyika Mafinga huku jumla ya mashauri 28 kati ya mashari 42 yaliyopangwa kusikilizwa kumalizwa, hata hivyo alisema kuwa mashauri mengine yaliyobaki yapo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kuyatolea maamuzi.
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa wamejiwekea utaratibu wa kukagua Mahakama na utendaji kazi wake pindi wanapomaliza kufanya kikao maalum katika sehemu husika, hali ambayo huwawezesha kujua changamoto na mafanikio mbalimbali yaliyopo katika maeneo hayo, lengo kuu likiwa ni kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Hata hivyo Mahakama ya Tanzania kupitia Maafisa wake imekuwa na utaratibu wa kufanya kaguzi za mara kwa mara kwa nyakati tofauti kwa lengo la kufuatilia kwa karibu kuona hali ya utendaji wa Mahakama mbalimbali kama zinaendana na matakwa ya Mhimili huu muhimu wenye dhamana ya kutoa haki kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment