Thursday, June 8, 2017

MMOJA APIGWA RISASI RUFIJI NA WAWILI WAOKOTWA WAKIWA WAMEKUFA

1
Nurdin Mohammed Kisinga ,anaedaiwa kupigwa risasi ya kichwa huko kijiji cha Ngomboroni kata ya Umwe Kaskazini,Ikwiriri wilayani Rufiji,akipatiwa matibabu.
………………….
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Nurdin Mohammed Kisinga ,amejeruhiwa baada ya kupigwa risasi ya kichwa ,na watu wasiojulikana huko kijiji cha Ngomboroni kata ya Umwe Kaskazini,Ikwiriri wilayani Rufiji.
Katika hatua nyingine watu wawili wenye jinsia ya kiume,wameokotwa wakiwa wamefariki dunia wilayani Rufiji na mwingine Kibiti.
Akielezea tukio la kupigwa risasi ,mkuu wa wilaya ya Rufiji,Juma Njwayo,alisema limetokea saa saba mchana, june 7 wakati Kisinga ,akiwa shambani kwake akivuna ufuta .
Alisema mtu huyo amejeruhiwa licha ya watu kudai kwamba ameshafariki dunia hivyo kama kutakuwa na taarifa nyingine zitatolewa.
Matukio hayo yametokea siku chache baada ya IGP Simon Sirro kwenda kuongea na wazee wa eneo hilo na mwenge wa uhuru kupita kutembelea miradi wilayani Kibiti na Rufiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, kamishna msaidizi mwandamizi,Onesmo Lyanga alithibitisha kuwa mtu huyo amepigwa risasi lakini amesita kukiri kuweka wazi kama tayari amefariki dunia.
Alisema anachofahamu Kisinga ,amejeruhiwa kwa risasi ya kichwa na watu wasiojulikana ambao bado wanatafutwa .
Ni siku moja tu,mkazi wa Rufiji,Eric Mwarabu ambae alikuwa ni askari mgambo alifariki mara baada ya kupigwa risasi nyumbani kwake.
Wakati huo huo maiti ya mwanaume ambae hajajulikana jina hadi sasa imeokotwa mchana june 7 huko kijiji cha Mtunda A,kitongoji cha Ngwaro,kata ya Mtunda wilaya ya Kibiti.
Katibu wa Chama Cha Mapinuzi CCM ,kata ya Mtunda ,Abdallah Mayonjo alieleza,maiti hiyo iliokotwa majira ya saa 11 june 6 ikiwa imefungwa kamba mikononi na miguuni na watu wasiojulikana .
Hata hivyo,mtu mwingine ameokotwa akiwa amefariki dunia kijiji cha Kipoka ,Ikwiriri wilayani Rufiji  huku ikiwa haina nguo.

No comments:

Post a Comment