Thursday, March 14, 2013

WANACHUO WA AFRIKA MASHARIKI KUJADILIANA FURSA ZA AJIRA KATIKA ENEO LAO.




Na Johary Kachwamba na Eleuteri Mangi _MAELEZO
WANACHUO Shule za biashara kutoka vyuo vikuu nane (8) mbalimbali  vya Afrika Mashariki wanatarajia kukutana ili kujadili fursa za ajira katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.



Kauli hiyo ilitolewa jana (leo) jijini Dar es salaam na Rais wa Wanachuo wanasoma masomo ya Biashara (Dar es salaam University Finance Association -DUFA) Maximillian Msuya wakati wanaongea na waandishi  wa habari.

Alisema kuwa lengo la mkutano huo ni kuzungumzia maswala ya sekta ya  mafuta na gesi na vilevile watazungumzia mitaala ya elimu katika eneo la Afrika mashariki.



Msuya aliongeza kuwa mkutano huo utaangalia  namna  gani nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaandaa wataalamu katika soko la ushindani la ajira za kuajiriwa na zile kujiajiri wenyewe.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi  ya tarehe 16 mwezi huu, katika Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.

Rais huyo ametaja vyuo vitakavyoshiriki kuwa ni Chuo Kikuu cha Nairobi (UON), Chuo Kikuu cha  Kisii na United States International University (USIU) kutoka Kenya.

Vingine ni Chuo Kikuu  Ndejje kutoka Uganda na kwa upande wa Tanzania kutakuwa na  Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na wenyeji Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam.

Mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stegomena Tax.

No comments:

Post a Comment