Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA) kinachoandaa bonanza la Waandishi wa Habari Tanzania, Juma
Pinto (kushoto) akizungumzia maandalizi kuhusiana na tamasha hilo
linalojulikana kama Media Day Bonanza. Katikati ni Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris
Malulu na kulia ni Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo Ally Choki.
Kiongozi wa kundi la Extra Bongo Ali Choki akiwa na wasanii wake.
Super Nyamwela akiongoza wananguaji wa kundi hilo kuonesha vionjo vitakavyoletwa na kundi hilo.
Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo Ally Choki
akizungumza na waandishi wa habari, pamoja nae ni wa TBL, Doris Malulu
******* *******
Na Mwandishi Wetu
BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo na kundi
la taarabu la Jahazi Modern ndiyo burudani zitakazonogesha tamasha la vyombo
vya habari litakalofanyika Dar es Salaam kesho (Jumamosi).
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa
kutambulisha burudani hizo, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA) kinachoandaa bonanza hilo, Juma Pinto alisema
maandalizi kuhusiana na tamasha hilo linalojulikana kama Media Day Bonanza
yamekamilika.
Alisema wameichukua Extra Bongo inayoongozwa na
Ally Choki na Jahazi Modern inayoongozwa na Mzee Yusuph kutokana na makundi
hayo kuwa juu hivi sasa katika muziki kwa maeneo yao.
“Tunaamini watakaokuja kwenye tamasha watakuwa
na furaha ya aina yake na tumejiandaa vya kutosha,” alisema Pinto na kueleza
kuwa bonanza hilo litafanyika viwanja vya Sigara Chang’ombe, Dar es Salaam na
mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Pia Pinto alisema bendi ya Msondo Ngoma Music
itapiga kwenye viwanja hivyo kuanzia saa moja usiku baada ya bendi za Extra
Bongo na Jahazi kumaliza kutumbuiza Media Day na kwamba imetoa ofa kwa
wanahabari watakaotaka kubaki kuendelea kupata burudani mpaka usiku wa manane.
“Msondo wana bonanza lao kila Jumamosi, sasa wamekubali kwamba wanahabari watakaotaka kubaki baada ya bonanza kumalizika jioni wabaki wajiunge na Msondo Ngoma,” alisema Pinto.
Bonanza hilo la TASWA linadhaminiwa na Kampuni
ya Bia Tanzania (TBL) likiwa na lengo la kuwaweka pamoja waandishi wote wa
habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine pamoja
na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kubadilishana mawazo na
kufurahi pamoja.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa TBL, Doris
Malulu alisema wamejipanga vya kutosha na kwamba wadau wafike kwa wingi
kuhakikisha mambo yanaenda kama yalivyopangwa.
“TBL ni mdau mkubwa wa wanahabari, tumewaandalia
mambo mazuri, naomba msikose,” alisema Malulu na kuongeza kuwa wanaamini wadau
1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari wanaotarajiwa kushiriki bonanza hilo
watafurahi vya kutosha siku hiyo.
Naye Choki akizungumza kwenye mkutano huo,
alisema vijana wake wamejipanga vya kutosha kushambulia na kuwa dhamira yao ni
kuona wana habari wanafurahi vya kutosha na kuwa mambo waliyowaandalia kila mtu
atafurahi kuiona Extra Bongo.
No comments:
Post a Comment