RPC ShinyangaJESHI la Polisi mkoani Shinyanga juzi lilizuia maandamano ya watoto na wanaharakati wa vikundi vya kutetea haki za binadamu.
Maandamano hayo yalipangwa kuanzia Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kupitia Kanisa Katoliki hadi makaburi ya Majengo mjini hapa ili kumzika mtoto yatima, Rose Doto (12) aliyeuawa kikatili hivi karibuni na kutupwa kwenye dampo la taka la Ngokolo Mitumbani.
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Evarest Mangala alikiri kuzuiliwa kwa maandamano hayo. Alisema yalizuiwa kwa sababu za kiusalama, kwa vile itakuwa si vyema kila mtoto anayeuawa, kuzikwa kwa maandamano.
Badala yake, alisema polisi waliruhusu maziko ya mtoto huyo, yafanyike kama maziko mengine, kwa kufuata taratibu zote za maziko.
Rose alipigwa na kitu kizito kichwani na mwili wake kufungwa kwa kamba ndani ya kasha na kutelekezwa kwenye dampo la Ngokolo Mitumbani. Kulikuwa na msafara wa kimya kimya wa magari na watembea kwa miguu katika maziko hayo.

Msafara huo ulianzia Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga hadi makaburini kwa kupitia Kanisa la Moyo Safi wa Maria, ilikofanyika ibada ya kumuombea marehemu.
Akizungumza na mamia ya waombolezaji kwenye makaburi ya Majengo, baada ya maziko ya mtoto huyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila alitoa mwito kwa jamii kukemea na kulaani vitendo vya kinyama na kikatili wanavyofanyiwa watoto, ambavyo huwasababishia madhara mwilini na hata vifo.