Tuesday, July 9, 2013

Jeshi latoa onyo kali kwa waandamanaji Misri


Waandamanaji wakikabiliana na Jeshi nchini Misri

Jeshi la Misri limetoa onyo kali, kwa yeyote ambaye ana nia ya kuvuruga usalama na uthabiti wa taifa hilo wakati huu nchi hiyo unakumbwa na mzozo wa kisiasa.
Waziri wa Ulinzi Abdel Fatah al-Sisi amesema hatma ya taifa hilo siku sijazo ni muhimu sana na kamwe hawataruhusu vurugu au uchochezi wa aina yoyote.

Wafuasi wa rais Morsi wamekuwa wakiandamana tangu rais huyo alipoondolewa madarakani.Tangazo hilo limetolewa wiki moja tu, baada ya jeshi la nchi hiyo kumuondoa madarakani rais Mohamed Morsi na kumteua jaji mkuu Adly Mansour kuwa kaimu kiongozi wa taifa hilo.
Awali, maafisa wakuu wa chama cha Muslim Brotherhood, wamepinga vikali pendekezo la rais wa mpito Adly Mansour kuweka ratiba ya kuandaa uchaguzi mkuu mwaka ujao.
Wanajeshi wa Misri wakishika doria
Mmoja wa viongozi wa chama hicho, Essam al-Erian anasema kuwa mpango huo utakaojumuisha mabadiliko ya kikatiba na kura mwaka ujao unarejesha nchi hiyo ilipokuwa baada ya mapinduzi ya kumwondoa mamlakani Hosni Mubarak.

Rais wa mpito alitangaza kuwa uchaguzi utafanyika mwaka ujao katika juhudi zake za kutuliza maandamano na hali ya taharuki nchini humo.
Tangazo hilo lilitolewa wakati mgogoro ukizidi kati ya jeshi na wafuasi wa rais aliyepinduliwa Mohammed Morsi karibu na kambi ya jeshi mjini Cairo ambako zaidi ya watu 50 waliuawa hapo jana wakati wa mapigano na wanajeshi.
Aidha tangazo la Rais Adly Mansour, linaashiria mageuzi katika katiba kwa kuitisha kura ya maoni ambayo huenda ikachangia kufanyika kwa uchaguzi mwaka ujao.

Watu zaidi wauawa

Hii inakuja wakati ambapo watu 51 wamethibitishwa kuuawa mjini Cairo.
Chama cha Muslim Brotherhood kinasema kuwa wanachama wake walipigwa risasi wakati walipokuwa wanakesha nje ya makano ambapo Morsi anazuiliwa, lakini jeshi linasema liliwafyatulia risasi kwani waandamanaji nao walikuwa wamejihami.
Rais Morsi, aliyekuwa rais wa kiisilamu na wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, aliondolewa mamlakani na jeshi wiki jana baada ya maandamano makubwa ya kumpinga kufanyika.
Wafuasi wake wanatuhumu jeshi kwa kufanya mapinduzi, lakini wapinzani wake wanasema hatua hiyo ni mwendelezo wa mapinduzi yaliyomwondoa mamlakani aliyekuwa rais Hosni Mubarak mwaka 2011.
Amri hiyo inasema kuwa jopo la kufanyia katiba marekebisho ambalo lilifutwa kazi wiki jana, litaundwa tena katika kipindi cha siku 15.
Mabadiliko hayo kisha yatapigiwa kura ya maoni. Mchakato utapangwa kufanyika katika muda wa miezi minne.
Baada ya kura ya maoni , uchaguzi wa wabunge huenda ukafanyika mapema mwaka 2014.
Hatimaye uchaguzi utafanyika punde baada ya bunge jipya kuundwa.

No comments:

Post a Comment