Monday, September 9, 2013

NI MWAKA MMOJA SASA TANGU KUUAWA KWA MWANGOSI NA MASWALI BADO HAYAJAPATA MAJIBU.


























NA MWANDISHI WETU.

Mwaka mmoja baada ya mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha luninga cha Channel ten Daudi Mwangosi  serikali imelaumiwa kwa kutofanya juhudi za kutosha kuchukua hatua kali kwa wahusika wa tukio hilo na kulinda maisha ya waandishi wa habari.

Mwangosi aliuawa akiwa mikononi mwa polisi Jumapili ya tarehe 02 Septemba, mwaka jana katika kijiji cha Nyololo wilayani Wilayani Mufindi  Mkoani Iringa katika tukio ambalo linaelezwa serikali ilikuwa imedhamiria kuficha ukweli wa hali halisi mpaka picha zilipopatikana kuthibitisha vinginevyo.

Wadau waliohudhuria kongamano la kumbukumbu ya mwaka mmoja baada ya mauaji ya Mwangosi lililoandaliwa na klabu ta waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza (MPC) na umoja klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) wamesema pamoja na kuwa mauji hayo yalitokea mikononi mwa Polisi hatua zinazochukuliwa ni kama serikali haioni athari za tatizo hilo kwa ustawi wa demokrasia na uhuru wa kujieleza nchini.

"Mimi sioni Kama serikali inahangaika, wako wametulia kama  vile kilichotokea ni kitu cha kawaida tu, hakuna uwajibikaji wa kutosha" anasema Paul Mabuga kutoka Sahara Media Group.


Baada ya mauaji hayo pamoja na kuwa ushahidi wa picha ya tukio hilo unaonyesha kuwa Marehemu Mwangosi alikuwa amezingirwa na askari polisi wengi lakini ni mmoja tu aliyeshitakiwa ambaye naye amekuwa akipelekwa mhakamani kwa kuficha sura ili asipigwe picha.

Pamoja na kunyooshewa kidole huko, serikali imeelezwa kutokuwa na dhamira njema toka mwanzo kwa kuwa tayari jeshi la Polisi lilishaundanganya umma wa Watanzania kuhusu tukio hilo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi Advera Senso  alinukuwaliwa akisema baada ya mauaji hayo kuwa Mwandishi alikuwa akikimbia kutoka upande wananchi na kuelekea walipokuwa Polisi na kwamba  inasemekana alipigwa na kitu ambacho mpaka sasa hakijafahamika bado mpaka uchunguzi ufanyike. Alisisitiza kuwa kuna kitu kilirushwa kikitokea upande wa Wananchi na kumfikia ambacho kilimjeruhi pia Askari akiwamo Mkuu wa kituo cha Polisi.

"Kama isingekuwa zile picha ina maana kulikuwa na hatua za makusudi kabisa kuficha ukweli wa nani muuaji, hata ugoi goi wa kufuatilia suala hili unatokana na msingi huo, hawakutaka tuujue ukweli, agenda yao sijui ilikuwa nini, lakini kitu kimoja wanatakiwa wajue ni ukweli kwamba haturudi nyuma." alisema mwandishi George Ramadhan.


Afisa mmoja mstaafu wa jeshila la polisi ameliambia Raia Mwema kuwa serikali imekosa umakini na hekima za kushughulikia mauaji hayo  kwa kuamua kupuuza zana ya uwajibikaji na dhamana ya madaraka wanayopewa viongozi wa umma. Kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama kumpadisha cheo aliyekuwa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa wakati mauaji yanatokea akiwa eneo la tukio kinaashiria kutojali maana ya dhamana za uongozi na kupuuza uzito wa mauaji hayo.



"Hata kama kulikuwa na mpango wa kumpadisha cheo busara za uongozi zinataka baada ya tukio mpango huo ungeishia hapo, hata kama hakuamrisha yeye lakini anawajibika kwa kuwa ana dhamana ambayo inamuwajibisha pia kwa makosa ya wasaidizi  wake, nyie vijana mnasahau Mzee Mwinyi (Raia mstaafu Ally Hassan Mwinyi) aliwajibika kwa makosa ya Polisi waliofanya huko Shinyaga" alisema mstaafu huyo na kuomba asitajwe jina gazetini.


Mwezi Mei mwaka huu Amiri Jeshi wa majeshi ya ulinzi usalama Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimpandisha cheo aliyekuwa kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda kutoka Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kuwa Naibu Kamishna wa Polisi (DCP)  kitendo ambacho kilalamikiwa na watu wengi kwa kuwa kingeweza kutafsiriwa kuwa serikali inampongeza baada ya mauaji hayo kutokea.

Katibu Jukwaa la wahariri Neville Meena alinukuliwa wakati huo na vyombo vya habari akieleza masikitiko yake kwa kitendo hicho.

“Hata kama hakuua yeye, lakini kwa matukio haya hasa hili la Mwangosi kwa sababu alikuwepo tangu mwanzo hadi mwisho wa tukio, tulitegemea aondoke na si kupandishwa cheo. Kuwepo kwake kumeendelea kutuumiza katika tukio zima, hakuchukua hatua kuzuia hata alipoambiwa. Inaonekana kwao ni utendaji kazi bora kulingana na walivyotaka. Wametusaidia kujua sisi waandishi kuwa tuanze kuitazama serikali kwa jicho la namna gani." alikaririwa katibu huyo.

UTPC na tuzo ya Mwangosi
Katika kumbukumbu hiyo Mkurugenzi mtendaji wa UTPC Abubakar Karsan alisema umoja huo umeanzisha mfuko David Mwangosi support and development fund ambao wanapanga kuutafutia shilingi bilioni tatu kwa ajili ya kusaidia waandishi wanaopatwa na matatizo kazini.



Sehemu ya mfuko huo ndiyo utakaokuwa ukitoa tuzo ya Daud Mwangosi kwa mtu aliyetoa mchango mkubwa na uliotukuka katika kuendeleza tasnia ya habari nchini. Tuzo hiyo itaambatana na zawadi pesa taslimu shilingi milioni 10.

Kwa mara ya kwanza  tuzo itatolewa Mwezi Oktoba mwaka huu wakati wa mkutano mkuu wa UTPC utakaofanyika jijini Mwanza, ambapo pia familia ya Marehemu Daud Mwangosi itahudhuria katika shughuli hiyo.

Tofauti na tuzo zingine Karsan amesema tuzo hiyo haitashindaniwa kwa waandishi wa habari kuandika habari au makala, isipokuwa mshindi wa tuzo hii atateuliwa na  kamati ya wataalam waliobobea katika taaluma ya habari ambao tayari wanafanya hiyo ya kutambua wasifu wa watu mbali mbali kulingana na vigezo vya tuzo hiyo na kumteua mshindi. Kamati inaundwa na Nkwabi Ng'wanakilala, Leila Sheikh, Rose Mwakitwange na Hamza Kasongo 



Waandishi msife moyo
Mkurugenzi wa asasi isiyokuwa ya kiserikali ya Governance Links inayojihusisha na masuala ya utawala bora Donald Kasongi alisema jamii yetu ni muhimu iendelee kuandaa watu kama Mwangosi ili kujenga utamaduni wa uwazi katika kuwahabarisha Watanzania.

"Tutumie nafasi hii kuanisha tumejifunza nini kutoka kwake na tutaenzi na kuyatumia vipi tuliyojifunza kushawishi na kusaidia kufanya Tanzania kuwa mahali salama na pa kujivunia katika tasnia ya habari. Natumaini mtakubaliana na mimi kuwa fundisho kuu kutokana na maisha pamoja na kifo cha Marehemu Daudi Mwangosi  ni kuwa na Natumaini" alisema.

Tukio la kuuawa kwa Mwangosi mwaka mmoja uliopita liliitia doa doa jeusi hadhi ya Tanzania kaimataifa ambapo ripoti ya Uhuru wa vyombo vya habari kwa kila nchi Duniani ( Press Freedom Index) inayotolewa na taasisi ya Waandishi waliokuwa na mipaka ( Reporters without Borders) inayonyesha kuwa Tanzania imeshuka nafasi 36 kutoka nafasi ya 34 mwaka 2011 mpaka kufikia nafasi ya 70 ndani ya  kipindi kifupi cha miezi minne.
















SOURCE G SENGO BLOG

No comments:

Post a Comment