Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa mkandarasi wa Kampuni ya Chongqing Foreign Trade and
Economic Cooperation (Group) kutoka China anayejenga barabara ya
Tabora-Nyahua yenye urefu wa KM 85 alipokagua kipande cha barabara ya
Tabora mjini chenye urefu wa KM 6, mkoani Tabora.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipokea
taarifa ya maendeleo ya mradi wa barabara ya Tabora-Nyahua kutoka kwa
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng.
Damian Ndabalinze, alipokagua kipande cha barabara ya Tabora mjini
chenye urefu wa KM 6.
Meneja
wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng. Damian
Ndabalinze, akionesha hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Tabora-
Sikonge (Usesula) yenye urefu wa KM 30 kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Tabora- Sikonge (Usesula) yenye urefu wa KM 30 ikiwa katika hatua ya awali ya ujenzi wake.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa mkandarasi wa kampuni ya Chongqing International
Construction Corporation (CICO), kutoka China anayejenga barabara ya
Tabora- Sikonge (Usesula) yenye urefu wa KM 30 alipokagua ujenzi wake.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
WAZIRI
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ametoa wiki
mbili kwa mkandarasi wa Kampuni ya Chongqing International Construction
Corporation (CICO), kutoka China anayejenga barabara ya Tabora- Sikonge
(Usesula) yenye urefu wa kilometa 30 kuongeza vifaa vya ujenzi katika
eneo la mradi na kuhakikisha ujenzi wake unatekelezwa kwa kasi na
kukamilika kwa wakati.
Akizungumza
mara baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na kasi
ya utekelezaji wake profesa Mbarawa amemtaka Mkandarasi huyo
kutumia kipindi cha muda wa ziada cha utekelezaji wa mradi huo
kilichoongezwa kukamilisha.
“Siridhishwi
na kasi unayoendelea nayo, kama hautatekeleza agizo hili haraka
iwezekanavyo nitasitisha mkataba huu mara moja na usitegemee kupata
mradi mwingine wa barabara nchini”, amesema Profesa Mbarawa.
Aidha,
Profesa Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa mradi huo uende sambamba na
viwango bora vya barabara vilivyomo kwenye mkataba uliosainiwa.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mbarawa amekagua barabara ya Tabora – Nyahua
yenye urefu wa kilometa 85 kipande cha barabara ya Tabora mjini chenye
urefu wa kilometa 6 kinachojengwa na kampuni ya Chongqing Foreign Trade
and Economic Cooperation (Group) kutoka China na kumtaka mkandarasi
kukamilisha barabara hiyo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
“Mpaka
mwezi Disemba nataka barabara hii iwe imekamilika kwa kiwango cha lami,
wananchi wa eneo hili wamekuwa wakiisubiri kwa hamu, hivyo hakikisha
unaikamilisha”, amesisitiza Prof Mbarawa.
Naye
Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Tabora Eng.
Damian Ndabalinze amesema kuwa wakala utamsimamia mkandarasi na
kuhakikisha vifaa vinaletwa katika eneo la mradi ndani ya mwezi huu.
Ameongeza kuwa mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa madaraja makubwa mawili na unagharimu zaidi ya Bilioni 28.
Kukamilika
kwa ujenzi wa miradi hiyo miwili kutafungua fursa nyingi ikiwa ni
pamoja na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika maeneo ya
kati na Magharibi mwa nchi yetu.
Waziri
Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Tabora
kukagua miundombinu ya barabara, uwanja wa ndege, reli na mawasiliano.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment