Thursday, October 17, 2013

Makamu wa Rais mpya Burundi



Busokoza alikuwa mfanyabiashara baada ya kustaafu kutoka katika jeshi
Nchini Burundi, Bwana Bernard Busokoza wa kabila wa watutsi na anayetoka chama cha Uprona, ameteuliwa kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi .
Bernard Busokoza mwenye umri wa miaka 60 , anachukua nafasi ya Terence Sinunguruza aliyejiuzulu hivi karibuni baada ya kupoteza imani ya chama chake cha Uprona kwa madai kwamba alipuuza maslahi ya chama na kujiendeleza yeye binafsi.

Busokoza alikuwa afisaa wa zamani wa jeshi la zamani la Burundi baada ya kupata elimu ya kijeshi nchini Ugiriki. Hata hivyo alijihusisha na maswala ya biashara hasa katika sekta ya mawasiliano baada ya kustaafu kutoka katika jeshi.

Anamiliki mojawapo ya kampuni kubwa ya mawasiliano nchini humo.
Uteuzi huo wa Bernard Busokoza umeidhinishwa Jumatanojioni na bunge pamoja na baraza la seneti.

Hata hivyo kulikuwa na pingamizi kuhusu uteuzi wake hasa kutoka kwa wabunge wa chama cha (CNDDFDD) cha Rais Pierre Nkurunzinza wakisema kuwa aliwahi kuhusika na mapinduzi ya kijeshi yaliyosababisha kifo cha rais wa kwanza wa kihutu Milkior Ndadai
Makamu wa rais aliyemtangulia, Terence Sinunguruza alijiuzulu kutokana na shinikizo za wanachama wenzake wa (UPRONA) waliodai kuwa haonekani kutetea masilahi ya chama chake.
Chama hicho kilimtaka Rais Pierre Nkurunziza kumfuta kazi Sinunguruza, aliyetuhumiwa kwa kusababisha migawanyiko chamani tangu kuchukua wadhifa huo miaka mitatu iliyopita.

No comments:

Post a Comment