JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA KAZI NA AJIRA
TAMKO LA SERIKALI KUHUSU KUSITISHA UTARATIBU WA KUKODISHA WAFANYAKAZI UNAOFANYWA NA BAADHI YA WAKALA BINAFSI WA HUDUMA ZA AJIRA
1. Wizara ya Kazi na Ajira imekua ikipokea malalamiko toka
kwa wadau mbalimbali kuhusu utaratibu wa udalali wa kukodisha
wafanyakazi katika makampuni unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa
Huduma za Ajira nchini.
2. Wizara
imefanya uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na kubaini kuwa utaratibu
wa kukodisha wafanyakazi unaofanywa na baadhi ya Wakala Binafsi wa
Huduma za Ajira ni kinyume cha Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya Mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002]. Kwa mujibu wa Kifungu 4 cha
Sheria hii, majukumu ya msingi ya Wakala wa Huduma za Ajira ni
kuwaandaa na kuwaunganisha Watafuta Kazi na Waajiri kwa kutoa mafunzo na ushauri elekezi kwa watafuta kazi, kutafuta fursa za ajira na kutoa taarifa za soko la ajira. Hivyo, Mawakala hawapaswi kuwa waajiri wa wafanyakazi waliowatafutia kazi kwa niaba ya Waajiri wengine.
3. Aidha, uchunguzi umebaini kwamba utaratibu
huu ni ujanja unaotumiwa na baadhi ya Waajiri na Mawakala kwa lengo la
kukwepa kodi na kujipatia faida kwa kukwepa kutoa haki za msingi za
wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria za Kazi. Baadhi ya makampuni
yanayokodisha wafanyakazi yamefanyiwa uhakiki na TRA na kubainika
kukwepa kodi ya mapato ya ajira (PAYE) na na kodi ya mapato ya kampuni kinyume na Kifungu cha 7 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ya Mwaka 2004 [Sura 332 kama ilivyorejewa Mwaka 2008].
4.Uchunguzi huu umebaini athari mbalimbali kwa wafanyakazi wanaoajiriwa kwa utaratibu huu. Athari hizo ni pamoja na:
· Wafanyakazi
kukosa haki ya hifadhi ya jamii kama vile likizo ya uzazi na matibabu
kinyume na Sheria mbalimbali za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii;
· Uwepo wa ubaguzi katika malipo ya mishahara kwa kazi ya aina moja kinyume na kifungu
cha 7(10) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004
ambacho kinamtaka mwajiri kuchukua hatua stahiki kwa kuhakikisha kuwa
wafanyakazi bila kujali jinsia zao wanalipwa mishahara linganifu na ya
haki kwa kazi yenye uzito na thamani sawa;
· Kukosa fursa za kujiendeleza kielimu na mafunzo;
· Kukosekana kwa usalama na uhakika wa ajira ;
· Wafanyakazi kulipwa mishahara ya kima cha chini kinyume na sekta wanayofanyia kazi.
5. Kwa taarifa hii, Wizara ya Kazi na Ajira imeamua kusitisha mara moja utaratibu wa Mawakala kuwaajiri wafanyakazi wanaowatafutia kazi. Aidha, Mawakala na Kampuni husika waliopo katika utaratibu huu kwa sasa wanapaswa kuwahamisha wafanyakazi waliokodishwa kutoka kwa Wakala kwenda kwa
Kampuni husika. Waajiri na Wakala wanatakiwa kukamilisha zoezi hili
ndani ya kipindi cha mwezi mmoja na kuwasilisha taarifa za utekelezaji
kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira kabla au ifikapo tarehe 28/02/2014.
6. Uchunguzi
zaidi unaendelea kubaini kama kuna wafanyakazi wa Kigeni wanaohusishwa
katika utaratibu wa kukodishwa ili hatua zinazotahili ziweze kuchukuliwa
ikiwa ni pamoja na kuwataka waombe vibali vya ajira kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji Na.7 ya mwaka 1995 na Sheria ya Huduma za Ajira Na.9 ya mwaka 1999. Wageni watakao kidhi vigezo wataajiriwa na kampuni walipokodishwa; ambazo kwa wakati huo zitakua ndiyo mwajiri wao.
7. Wizara
ya Kazi na Ajira inawaelekeza Wakala wa Huduma za Ajira nchini kwamba,
kwa utaratibu wa sasa watapaswa kuwasilisha barua za maombi ya usajili wa Uwakala kwa KAMISHNA WA KAZI kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Ajira Na. 9 ya mwaka 1999 [Sura 243 kama ilivyorejewa Mwaka 2002]
ili waweze kufanya shughuli za Uwakala wa Huduma za Ajira kisheria.
Maombi haya yawasilishwe ndani ya kipindi cha mwezi mmoja tangu kutolewa
kwa tangazo hili. Baada ya muda huo Wakala asiye na kibali cha Kamishna
wa Kazi hatoruhusiwa kuendesha shuguli za huduma za ajira nchini.
Aidha, Mawakala watakaopata leseni ya Kamishna wa Kazi yatakua yakitangazwa ili yatambuliwe na Umma.
8. Nasisitiza, maelekezo haya yatatolewa kwa Makampuni na Wakala waliohusishwa katika uchunguzi kwa ajili ya utekelezaji.
IMETOLEWA NA
GAUDENTIA MUGOSI KABAKA (MB)
WAZIRI WA KAZI NA AJIRA
27/01/2014
No comments:
Post a Comment