Katibu
wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandihi wa habari
katika Ukumbi wa Sekretarieti ,Makao Makuu ya CCM Ofisi Ndogo Lumumba.
..................................................................................
Mara
baada ya kuundwa kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
inayoongozwa na Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana mwanzoni mwaka mwaka
jana, Sekretarieti hiyo imejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mikoani
kukutana na wananchi kusikiliza kero zao,kukagua utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM na kuimarisha Chama mikoani. Utaratibu huu ni agizo la
mkutano mkuu wa Taifa wa nane wa CCM uliofanyika Novemba 2012 mjini
Dodoma. Nanukuu azimio hilo;
“
Chama Cha Mapinduzi lazima kiwe karibu na wananchi, kisikilize
changamoto zao na kiwasemee wananchi na hasa wanyonge” Moja ya maazimio
ya Mkutano Mkuu wa nane wa CCM 2012.
Kwa
hiyo msingi wa kwanza wa ziara hizo ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa CCM
Taifa ambacho ndicho kikao cha juu kabisa cha Chama. Msingi wa pili ni
ukweli kuwa CCM ndio iliyopewa dhamana na kuingia mkataba na wananchi
kupitia ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015, hivyo inayowajibu
wa kukagua utekelezaji wa ilani hiyo.
Na
bila shaka wote tumeshuhudia jinsi ziara hizo zilivyoinua uhai wa Chama
nchi nzima na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na
kutatua kero mbalimbali za wananchi kwenye maeneo yao, kiasi cha
kuongeza imani ya wananchi kwa CCM.
Tumeshuhudia
makundi mbalimbali ndani ya jamii yakija kueleza changamoto zao ndani
ya Chama. Makundi hayo ni pamoja na makundi ya wakulima, wafugaji,
wafanyabiashara, wanafunzi na wafanyakazi hasa walimu. Huu ni
uthibitisho wa kuongezeka kwa imani yao kwa CCM.
Katika
mwendelezo wa ziara hizo mwishoni mwa mwaka jana Katibu Mkuu wa CCM na
baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti walifanya ziara ya siku 26 katika
mikoa ya Ruvuma, Mbeya na Njombe. Pamoja na mambo mengine wananchi
walilalamikia baadhi ya watendaji wa serikali hasa baadhi ya mawaziri
wakiamini kuwa yapo mapungufu kadhaa yanayotokea kwenye wizara zao.
CCM
kama lilivyo agizo la Mkutano mkuu la kuwasemea wananchi tulisikiliza
kilio chao na kwa kufuata utaratibu, baadhi ya mawaziri hao waliitwa na
kuhojiwa kwenye Kamati Kuu ya CCM mwezi Disemba 2013.
Utaratibu wa watendaji wa serikali kutoa taarifa za utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwenye vikao vya Chama sio mgeni na wala
haujaanza jana. Wakuu wa wilaya hutoa kwenye wilaya, wakuu wa mikoa
hutoa mikoani kwao,hivyo sio utaratibu mpya.
Baada
ya mahojiano hayo Kamati Kuu ya CCM ilitoa ushauri kwa serikali wa
namna ya kurekebisha mapungufu yaliyoelezwa na wananchi. Kwakuwa kwa
mujibu wa Katiba ya Nchi mwenye mamlaka na mawaziri ni Rais mwenyewe,
CCM ililiacha suala hili kwake aangalie njia ipi bora ya kuondoa
mapungufu tuliyoyaeleza.
Na
kwenye taarifa yetu kwa vyombo vya habari baada ya kikao hicho
tulisisitiza kuwa sio lazima awafukuze mawaziri husika isipokuwa
wanaweza kufanya mabadiliko katika mfumo,sheria nk ili mradi kuwepo na
mabadiliko katika kushughulikia mambo yaliyolalamikiwa na wananchi.
Hivi
karibuni Rais amefanya mabadiliko kidogo kwenye baraza lake la mawaziri
na kuwarudisha baadhi ya mawaziri waliolalamikiwa na wananchi na
wabunge, ambao malalamiko hayo yaliungwa mkono na CCM. Ni kupitia
malalamiko hayo ndipo lilipozaliwa jina la mawaziri mizigo. Baada ya
uteuzi huo kukaibuka mjadala mkubwa nchini wakihoji kulikoni Rais kaamua
kutowatimua mawaziri hao.
Kwanza
haikua hoja ya CCM kuwafukuza mawaziri hao bali kuchukua hatua za
kurekebisha mapungufu husika. Kufukuza inaweza kuwa ni njia ya kutatua
tatizo lakini sio njia pekee. Hivyo basi CCM tunaamini kuwa kurudishwa
kwao wamepewa fursa ya kurekebisha mapungufu tuliyoyasema kwa niaba ya
wananchi. Tunaamini mawaziri wote hawatabweteka bali watatimiza wajibu
wao na kuhakikisha wanawatumikia wananchi ambao ndio waajiri wa
serikali.
Ifahamike
kuwa Chama Cha Mapinduzi hakitasita kuchukua hatua kali dhidi ya
mawaziri na watendaji wengine watakaoshindwa kurekebisha mapungufu na
watakaoshindwa kutimiza wajibu wao vizuri. Wakumbuke kushindwa kwao
kutimiza majukumu yao ni hujuma kwa Ilani ya uchaguzi ya CCM, CCM
haitavumilia usaliti huo. Kukaa kimya kwa CCM itakua ni kujinyonga
yenyewe jambo ambalo hatutaruhusu kabisa.
Tunajua
wapo baadhi ya watendaji wa serikali wasiopenda kuhojiwa utendaji wao,
tunawasihi kwa moyo safi wasiotaka kuulizwa juu ya utendaji wao waondoke
serikalini wenyewe kwani CCM tutakuwa wakali sana kwenye
mapungufu,kwani tukikaa kimya tutakua tunajihujumu wenyewe.
Tutatumia
vizuri wingi wa wabunge wetu bungeni na wingi wa madiwani wetu kwenye
halmashauri kuisimamia vizuri serikali. Hivyo kuanzia sasa kasi ya CCM
kuisimamia serikali, kuisifu itakapofanya vizuri na kukosoa itakapofanya
vibaya itaongezeka mara dufu kwa kila ngazi.
Tunawaomba
watanzania kwa ujumla tuwape muda wateule hawa wa Rais watimize wajibu
wao, lakini tusisite kusema pale tutakapoona mambo hayaendi kama
tunavyotarajia. Uwajibikaji wa kweli ndio msingi wa mafanikio na
maendeleo yetu.
CCM
inawatakia kila lakheri kwenye kutimiza wajibu wao. Tuna matumaini
makubwa kuwa wote kwa pamoja hawataisaliti ilani ya Uchaguzi ya CCM na
kwamba hawatayaangusha matumaini ya wananchi kwa serikali yao.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
Nape Moses Nnauye
Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi
23/01/2014
No comments:
Post a Comment