Wakazi wa Tabata na viunga vyake, sasa wanaishi kwa wasiwasi
mkubwa kutokana na kuibuka kwa kundi la vijana, wanaojiita Waasi
wakitumia silaha za jadi, kujeruhi watu na kupora mali nyakati za usiku.
Mmoja wa wananchi wa Tabata Matumbi alisema wiki
mbili zilizopita, vijana hao walimuua mwanamume mmoja kwenye Daraja la
Reli la Matumbi. Kwa mujibu wa mtoa habari huyo ambaye hata hivyo
hakutaka jina lake litajwe, mtu huyo alichinjwa na kichwa chake
kutenganishwa na kiwiliwili.
“Watu walipeleka kiwiliwili kituo cha polisi,
maana kichwa hakikupatikana na haikufahamika kama alitambuliwa au vipi.
Yaani sasa hivi ikifika saa tatu watu inabidi tubaki ndani,” alisema.
Habari zilisema pamoja na mauaji hayo, pia kumekuwa na matukio ya watu kuvamiwa, kujeruhiwa na kuporwa mali zao.
Inasemekana vijana wanaofanya uhalifu huo ni wa umri wa kati ya miaka 14 na 17.
Mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Pima
alisema alivamiwa na kundi la vijana wasiyopungua kumi akiwa nje ya
nyumba yake.
Alisema vijana hao walimkata panga kichwani, baada ya
kutotii amri yao ya kutaka awakabidhi simu na kila alichokuwa nacho
mfukoni.
“Kwanza walipita watoto watatu, wakafuatiwa na
wengine watatu, mara akatokea mmoja na kunifuata barazani, akanitaka
nimpe simu, nikahisi anatania maana ni katoto,” alisema Pima.
Alisema ghafla walitokea wengine wawili na kumwamuru atekeleze amri mara moja.
Alisema mmoja alijaribu kumpokonya simu, lakini
akamwahi. Mtu huyo alisema hata hivyo kiongozi wao alimjeruhi kwa panga
kichwani.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msimbazi,
Beatrice Mukama alisema juzi baadhi ya wananchi wa kushirikiana na
polisi waliendesha msako uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa 16 .
Alisema watuhumiwa hao wamekabidhiwa polisi-Bunguruni
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment