Mtaalamu
kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mhandisi Dkt. Crispin Kinabo
akiwasilisha mada juu ya utunzaji wa mazingira kwenye migodi wakati wa
mafunzo hayo yaliyofanyika mapema leo katika wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma. Mafunzo hayo yalishirikisha viongozi na watendaji wa wilaya,
madiwani, wakuu wa vitongoji na wachimbaji wadogo lengo lake likiwa ni
kuwapa uelewa wa kanuni za uchimbaji bora wa madini.
Mmoja
wa wakilishi wa wachimbaji wadogo ambaye ni mmiliki wa mgodi katika eneo
la Mhesi Mapinduzi lililopo wilayani Tunduru Bi Sofia Hamdan akichangia
mada wakati wa mafunzo hayo.
Mpepo
Ismail ambaye ni mmoja wa wachimbaji wadogo na mmiliki wa machimbo ya
shaba Mbesa akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho. Ameitaka Serikali
kuangalia uwezekano wa kuwasaidia wachimbaji wadogo kwa kuwakopesha
vifaa vya kuchimba madini.
Baadhi ya washiriki wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa na watoa mada kwa nyakati tofauti (hawapo pichani).
Na Greyson Mwase, Tunduru
Wachimbaji
wadogo wametakiwa kuzingatia kanuni za usalama migodini ili kuepuka
majanga yanayoweza kujitokeza na kuleta athari kwa jamii kwa ujumla.
Hayo
yalisemwa na Afisa Madini Mkazi Tunduru Mhandisi Frederick L. Mwanjisi
alipokuwa akiwasilisha mada kwenye mafunzo yaliyoshirikisha wachimbaji
wadogo, viongozi na watendaji wa wilaya, madiwani na wenyeviti wa
vitongoji yanayoendelea wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Mhandisi
Mwanjisi alisema kuwa wachimbaji wengi wamekuwa wakithamini madini
kwanza badala ya mazingira kwa jamii inayowazunguka jambo
linalosababisha kujitokeza kwa majanga ya mara kwa mara kama vile
kuanguka kwa vifusi na kemikali kuathiri binadamu ikiwa ni pamoja na
wanyama.
“
Wachimbaji wamekuwa wakitanguliza msemo usemao “madini kwanza” kwa
kufikiria maslahi yao binafsi badala ya kufikiria jamii inayowazunguka
kwa kuweka mazingira katika hali ya usalama yaani msemo uwe “Usalama
kwanza” Alisisitiza Mhandisi Mwanjisi.
Mhandisi
Mwanjisi alibainisha athari zinazosababishwa na majanga yanayotokana na
kutokuzingatia usalama migodini ni pamoja na mmiliki kupoteza fedha
nyingi kwa ajili ya fidia, miundombinu kuharibika, kupoteza imani kwa
wafanyakazi na umma kwa ujumla hali inayoweza kupelekea hata mgodi
kufungiwa.
Aliendelea
kutaja athari nyingine kwa upande wa wafanyakazi kuwa ni pamoja na
kupoteza nguvu kazi, ulemavu wa maisha, kuathirika kisaikolojia ikiwa ni
pamoja na kukosa furaha ya maisha.
Mhandisi
Mwanjisi aliongeza kuwa jukumu la usalama kwenye migodi ni la wote
kuanzia wamiliki wa migodi, wafanyakazi, serikali ikiwa ni pamoja na
jamii inayozunguka migodi.
Mhandisi
Mwanjisi aliainisha kanuni za usalama migodini ikiwa ni pamoja na
uvaaji wa vifaa vya kujikinga na mazingira hatarishi, kuweka mgawanyo wa
kazi kulingana na taaluma na uzoefu wa wafanyakazi migodini, kufukia
mashimo ikiwa ni pamoja na kuwekea wigo maeneo hatarishi ndani ya
migodi.
Aliongeza
kanuni nyingine za usalama ni pamoja na kufanya ukaguzi wa maeneo ya
machimbo kabla ya kuanza kazi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa
mkaguzi wa migodi juu ya matukio ya hatari au ajali zinazotokea
migodini.
Kanuni
nyingine ni pamoja na kuwa na orodha ya wafanyakazi wote wa mgodi
katika daftari maalumu, vifaa vya huduma ya kwanza na kutoshirikisha
watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 katika kazi za machimbo.
Aidha
Mhandisi Mwanjisi aliwataka wachimbaji wadogo kuwa na mpango wa usalama
kwenye migodi wenye kuainisha tahadhari zinazoweza kuchukuliwa pindi
majanga yanapotokea katika migodi badala ya kutokuwa na mpango wowote
hali inayopelekea ugumu katika kushughulikia kwa haraka majanga
yanapojitokeza.
Wakati
huo huo mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Jiolojia
Mhandisi Dkt. Crispin Kinabo aliongeza kuwa wachimbaji wadogo mbali na
kuzingatia kanuni za usalama migodini wanatakiwa kufanya tafiti za
kijiolojia kabla ya kuanza uchimbaji wa madini ikiwa ni pamoja na kusoma
ramani za kijiolojia.
Dkt.
Kinabo aliwataka wachimbaji wadogo kuachana na uchimbaji wa mashimo
kiholela bila kusoma ramani za kijiolojia za maeneo husika hivyo
kupelekea kuwa na mashimo kila mahali na hivyo kupelekea majanga ya
kujitakia.
Aidha
Dkt. Kinabo aliwataka wachimbaji kuzingatia kanuni za mazingira kwa
kutunza vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na mpango wa kuotesha miti.
Mafunzo
haya yaliandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini lengo lake likiwa ni
kuwapa uelewa wa kanuni za uchimbaji bora wa madini wachimbaji wadogo
ikiwa ni pamoja na viongozi na watendaji wa wilaya, madiwani, wakuu wa
vitongoji na wachimbaji wadogo.
No comments:
Post a Comment