Monday, January 27, 2014

WANANCHI WA MTWARA WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA MAFUNZO

Na mwandishi wetu Mercy Edgra
MASASI MTWARA


Wananchi wa masasi wametakiwa kuchangamkia fursa za kuinua kipato zinapojitokeza, kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mafunzo mbalimbali ya kuinua uchumi yanapotolewa, ili kuweza kuinua hali zao za kiuchumi kwa kujiajiri.


Hayo yamesemwa na mwezeshaji wa mafunzo juu ya jinsi ya kuzalisha gesi itokanayo na kinyesi cha wanyama, Biogas Bi Faith Muhuri, alipokuwa anaongea na redio fadhila katika ufunguzi wa mafunzo ya  kutengeneza Biogas, yatayoendelea kwa siku 16 katika ukumbi wa Masista,migongo.


Akielezea faida ya gesi asilia inayotokana na kinyesi cha wanyama, Bi Faith Muhuri amesema kuwa pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, gesi hiyo inahifadhi mazingira na baada ya kutumika inakuwa mbolea na dawa ya kuua kupe na wadudu wengine wanaoharibu mazao.


Naye fundi ujenzi wa mitambo ya gesi asilia kutoka AB enterprises, bwana Adolfu Namtutu amewataka wananchi wa masasi na maeneo jirani, mafundi na wasio mafundi kujitokeza kwa wingi katika semina hiyo, ili wapate kuongeza kipato zaidi ikizingatiwa kuwa mafunzo hayo yanatolewa bure.


Mafunzo juu ya kutengeneza mitambo ya biogas yameanza jumatatu tarehe 27.1.2014, katika ukumbi wa masista, migongo na yatafanyika kwa siku 16, bila gharama yoyote ya mafunzo.

No comments:

Post a Comment